Mashujaa yafanya ushujaa ASFC

 TIMU ya Mashujaa ya mkoani Kigoma imeyaanza vizuri mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘ASFC’ baada ya kuichapa timu ya Mbuga FC ya mkoani Mtwara, mabao 3-2.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma wageni hao kutoka Mtwara walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na mchezaji wake, Haridi Ramsachi kipindi cha kwanza, dakika ya 8’ pasi ya Fadhili Waziri.

Mbuga FC ambao ni Mabingwa wa Mpira wa miguu Mkoa wa Mtwara walionekana kutawala mchezo huo kwa kipindi chote cha dakika 45 za kipindi cha kwanza na hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Mbuga FC ilikuwa mbele kwa goloi 1-0.

Mashujaa ilianza kipindi cha pili kwa kasi na dakika ya kwanza ya kipindi cha pili (dakika 46) walipata goli la kusawazisha lililofungwa na Kelegea Wazanga akimalizia pasi ya Athuman Makambo.

Kufuatia kuingia kwa goli hilo timu ya Mbuga FC iliongeza mashambulizi langoni mwa Mashujaa na kupata goli la pili lililofungwa na Azizi Chikoyo kwa kichwa akiunganisha krosi iliyopigwa kwenye goli la Mashujaa na kumshinda mlinda lango, Hashim Mussa wa Mashujaa.

Goli la pili la mabingwa hao wa Kusini, kuliwafanya Mashujaa kufanya mabadiliko ya wachezaji wake, ambayo yaliyozaa matunda kwenye dakika ya 54 kwa goli la penati lililofungwa na Ismail Mhesa aliyeangushwa ndani ya eneo la penalti na mchezaji wa Mbuga, Haridi Ramsachi.

 Dakika ya 65 Masome Mashauri aliipatia Mashujaa goli la tatu akimalizia pasi ya Ismail Mhesa ambapo hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa Mashujaa ilikuwa mbele kwa goli 3-2.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments