Serikali yazungumzia ushiriki wa Tanzania mkutano Dubai

DUBAI; SERIKALI ya Tanzania inashiriki Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), imesema mkutano huo ulianza Novemba 30, 2023 na utamalizika Desemba 12, 2023 , Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ambapo washiriki wakiwemo wakuu wa nchi na Serikali zaidi ya 81,000 kutoka nchi takriban 190 wanahudhuria mkutano huo.

“Ikumbukwe kwamba jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi zinahusisha wadau mbalimbali ikiwemo serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, vijana na watoto, hivyo, idadi kubwa ya Watanzania ilionesha nia ya kushirki katika mkutano huo wa kimataifa ambapo Jumla ya Watanzania 763 walijiandikisha kwa nia ya kushiriki.

“Kati ya idadi hiyo Watanzania 391 walijiandikisha kutoka wizara na taasisi za Serikali, wakati 372 walijiandikisha kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, sekta binafsi, vijana na watoto.

“Hata hivyo idadi ya Watanzania wanaoshiriki kutoka serikalini ni 66, ambapo hamsini na sita (56) wanatoka Tanzania Bara na 10 kutoka Zanzibar ambayo ni sawa na asilimia 8.7 ya Watanzania waliojiandikisha.

“Aidha, sehemu kubwa ya washiriki inatoka katika sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vijana na watoto ambayo ni 340, sawa na asilimia 91.3.

“Baadhi ya washiriki kutoka wizara na taasisi za Serikali wamefadhiliwa na mashirika ya Kimataifa aidha washiriki kutoka sekta binafsi, taasisi za kiraia, vijana na watoto wanashiriki kwa gharama zao wenyewe.Hii inaonyesha mwamko wa Watanzania kuhusiana na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi,” imesema taarifa hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments