TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU MAENDELEO YA HALI BAADA YA MAAFA WILAYANI HANANG,MKOA WA MANYARA.

Ifuatayo ni taarifa fupi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya leo Jumatano, tarehe 13 Desemba, 2023, kuhusu maendeleo ya hali baada ya maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang wilayani Hanang mkoani Manyara, yaliyotokea alfajiri ya tarehe 3 Desemba, 2023 kama ilivyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi.

TAARIFA YA VIFO.

Hakuna miili zaidi iliyopatikana hivi leo na hivyo idadi ya miili inabakia kuwa 89.
Miili 87 imetambuliwa na kuchukuliwa na familia zao kwa ajili ya mazishi lakini miili miwili ya watoto wa kike wa umri wa mwaka mmoja na miaka mitatu inafanyiwa vipimo vya vinasaba (DNA) ili kujiridhisha na utambuzi wake.
Bado utafutaji unaendelea.


Serikali inaendelea kugharamia mazishi na kutoa mkono wa pole wa kiasi cha shilingi milioni moja kwa kila mwili ikiwa ni agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

TAARIFA YA MAJERUHI.
Idai ya majeruhi inaendeelea kupungua ambapo hadi kufikia saa 9:00 alasiri tarehe 13/12/2023 walikuwa wamebakia majeruhi 15 kutoka idadi ya jumla ya 139 waliofikishwa hospitalini na kupatiwa matibabu.


Mgawanyo wao ni kama ifuatavyo: Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara majeruhi tisa (9); Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) majeruhi watatu (3); na Kituo cha Afya Gendabi watatu (3).


Matibabu ya majeruhi wote yanagharamiwa na Serikali kwa agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

KAMBI ZA WAATHIRIKA.


Hadi sasa wamebakia waathirika 96 tu wanaopatiwa huduma katika kambi za waathirika kama ifuatavyo: Shule ya Msingi Ganana ina waathirika 19; Shule ya Msingi Gendabi ina 52 na Shule ya Sekondari Katesh 25.


Serikali inaendelea kuwaunganisha waathirika na ndugu na jamaa zao. Kila mtu au kaya inayoondoka inapewa chakula na mahitaji muhimu ya kusaidia waendelee na maisha.


Hadi sasa waathirika 438 wa kaya 119 wameunganishwa na ndugu na jamaa zao na kuna mchakato wa kuzinganisha na ndugu zao kaya zingine 31 zenye watu 96.


MISAADA YA FEDHA, CHAKULA, VITU NA VIFAA.


Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu misaada fedha taslimu na vifaa kutoka kwa wahisani mbalimbali wa ndani na nje zikiwemo taasisi za umma na binafsi.
Tayari kufikia jana tarehe 12/12/2023 kiasi cha shilingi 149,757,500/- kilikuwa kimeingia kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa (National
Relief Fund) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Michango inaenedelea.


Aidha, mbali ya michango iliyopitia mfumo wa maafa, taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina zimeshachanga shilingi 2,100,000,000/- na kufanya jumla kuu ya fedha taslimu iwe shilingi 2,249,757,500/-.


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Hanang pia zinaendelea kupokea misaada ya chakula, vitu na vifaa mbalimbali ambavyo hadi sasa vimeshatolewa na wahisani 190 kama watu binafsi au taasisi na kampuni binafsi na za umma za ndani na nje ya nchi.


Hadi kufikia saa 6:30 mchana tarehe 12/12/2023 misaada hiyo ilikuwa imefikia thamani ya soko ya shilingi 1,899,058,221/-. Vitu vyote hivi vinahifadhiwa wilayani Hanang.


JUHUDI ZA SERIKALI:
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kusimamia suala la afya kwa umma na kuhakikisha magonjwa ya mlipuko hayatokei katika eneo lote lililoathirika na maafa haya. Juhudi hizo zinahusisha kuzitembelea kaya ambapo hadi sasa jumla ya kaya 5,410 zimeshafikiwa na dawa 102,405 za kutibu maji zimeshagawiwa.


Aidha, waathirika wengine 1,853 pia wameshapatiwa msaada wa kisaikolojia na timu ya wataalamu wa Wizara ya Afya wakiwemo wauguzi wawili na madaktari bingwa watatu wa afya ya akili na maafisa ustawi wa jamii 91 kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

WITO WA SERIKALI
Serikali inawashukuru na kuwapongeza Watanzania na taasisi mbalimbali za umma na binafsi ndani ya nchi yetu kwa moyo wa utu na uzalendo kwa kujitolea misaada mbalimbali. Serikali inatoa wito kwa misaada zaidi ya vifaa vya ujenzi ili viwasaidie waathirika kuanzisha makazi mapya.


Kamati ya Maafa ya Taifa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imetoa akaunti ya benki ya kuweka fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.

Akaunti hiyo ya kielektronikia ni National Relief Fund - Na. 9921159801na swift code TANZTZTX kwa wanaotuma fedha kutoka nje ya nchi.
Miamala inapotumwa inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG.
Akaunti hiyo ipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na inapokea fedha kutoka ndani na nje ya nchi.






TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments