Biteko awataka wananchi kuyaenzi Mapinduzi

 

ZANZIBAR: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuyaenzi, kuyalinda na kuyaishi kwa dhamira ya dhati, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwani Waasisi wa Nchi  walifanya mapinduzi hayo ili kuwa na taifa huru ambalo kila mtu anakuwa na haki, kuondoa dhuluma iliyokuwepo na kufanya wananchi kuishi kwa amani na furaha.

Amesema hayo Januari 06, 2024 wakati akizungumza na Wananchi  mkoani Kusini Pemba mara baada ya kuzindua Afisi ya uhamiaji na makazi ya askari wilayani humo.

“Sisi Wananchi tunawajibu wa kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kuyaishi, kuyaheshimu, kukuza uchumi wa nchi na kukuza uzalendo ili baada ya muda mrefu hata baada ya miaka 100 mbele, watakaokuja kusherehekea Mapinduzi haya wakute Zanzibar iliyobora zaidi na waseme Mapinduzi haya yalitufaa.” Amesema Dk. Biteko

Ameeleza kuwa, moja ya tunu tuliyonayo ni mshikamano hivyo watu wasiruhusu mtu yoyote kuwagawanya kwa misingi yoyote ile, bali maendeleo yaunganishe watu wote na kwamba tofauti za vyama, dini na  kabila visifanye watu wakae kwenye makundi bali kuunganisha watu kwa maslahi ya nchi na Watanzania.

Amesema kuwa, nchi inapoenda kusherehekea Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12 mwaka huu, watanzania wote waungane kuwaombea Rais ,Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ili waendelee kuongoza vyema, kuimarisha ustawi wa taifa na kuwaunganisha Watanzania.

Kuhusu Jengo hilo jipya la Afisi ya Uhamiaji Biteko amesema kuwa ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani kabla ya Mapinduzi watu walinyimwa haki zao za kimsingi zikiwemo za uhamiaji kama vile kupata pasi ya kusafiria na hivyo Mapinduzi yamewezesha wananchi kupata uhuru wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi.

Ameongeza kuwa, Ofisi hiyo ya Uhamiaji Wilaya ya Mkoani ilianza mwaka 1979 ikiwa ni ndogo lakini sasa kuna jengo la kisasa litakalowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa wilaya hiyo na viunga vyake, ikiwa ni kielelezo cha Mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amepongeza viongozi Wakuu wa nchi kwa juhudi wanazochukua ili wananchi wapate huduma bora ikiwa pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema anayoyafanya kwa vyombo vya usalama nchini ikiwemo kutoa vibali vya ajira, upandishaji vyeo, mafunzo, ulipaji madeni na kuwezesha vyombo vya usalama kwa kununua vitendea kazi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments