DKT. BITEKO ATAKA UMOJA WA VIJANA CCM KUSHIKAMANA KULETA MAENDELEO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo
tarehe 8 Januari, 2024 amefungua Kongamano la Umoja wa Vijana wa
Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho
ya kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kongamano hilo ambalo limefanyika katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa
Mjini Magharibi limeambatana na matembezi ya vijana nchi nzima
kuhamasisha umuhimu wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi
Maendeleo.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ni silaha
ya Chama katika uchaguzi na kupeleka maendeleo kwa wananchi na kwamba
CCM inaona fahari na heshima kubwa kuwa na vijana kama wao, “hata
uchaguzi ukija tuna uhakika nguvu kubwa ya ushindi ipo, nawapongeza
kwa kuweka rekodi na kuthibitisha kuwa mpo imara kwani rekodi hii bado
haijawekwa na chama chochote kile.”

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Zanzibar, amesema kuwa, kuna
mabadiliko makubwa na miradi inayofunguliwa ni mingi na kwamba, Rais
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi anafanya kazi
kubwa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan anaifanya katika kuwapelekea maendeleo wananchi hasa
walio maskini ili kuinua hali zao za kiuchumi na kuweka miundo mbinu
wezeshi ya kiuchumi.

Kutokana na juhudi hizo zinazofanywa na Viongozi Wakuu wa nchi katika
kuwaletea wananchi maendeleo, ameitaka UVCCM kuhakikisha wanawasaidia
viongozi hao katika kuyasemea mazuri wanayoyafanya tena bila kificho.

Katika utendaji kazi wa UVCCM, Dkt. Biteko ametoa angalizo kuwa, kwa
sasa kuna wasomi wengi nchini na mitandao yenye kuunganisha watu wengi
lakini suala hilo lisiwafanye waogope kutekeleza majukumu yao kwa kuwa
watakosolewa kwani kukosea kupo katika safari ya mafanikio.

Amepongeza matembezi ya vijana hao yaliyofanyika nchi nzima kwani
wamekipa uhai Chama na kudhibitisha kuwa CCM iko imara kupitia UVCCM.

Kongamano hilo la kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar
limehudhuriwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Komredi Mohamed Ally
Kawaida, Naibu Katibu Mkuu, UVCCM, Mussa Haji Mussa, Makamu Mwenyekiti
wa Chipukizi Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Wajumbe Jumuiya
ya Wazazi, Wenyeviti wa Mikoa wa UVCCM Tanzania, Makatibu wa Mikoa wa
UVCCM, Wenyeviti na Makatibu wa UVCCM ngazi ya wilaya nchi nzima na
Makatibu wa Hamasa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa ufunguzi wa  Kongamano la  Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Kongamano limefanyika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 8 Januari, 2024.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments