“Jitokezeni kutoa maoni miswada ya Sheria ya Uchaguzi”

 

MBOGWE, Geita: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika kutoa maoni kuhusu muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani  wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na  Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Dk Biteko amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita katika Sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

“Mheshimiwa Rais amepeleka miswada hii bungeni iliyosomwa wakati wa Mkutano wa 13 wa Bunge na tangazo limeshatoka la kuwaomba wananchi kwenda kutoa maoni yao bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari 2024  kuhusu marekebisho ya sheria hizi, niwaombe watanzania, nendeni mkatoe maoni yenu  ili kujenga Tanzania iliyo bora kuliko kubaki nyuma kulalamika,” amesisitiza Dk Biteko

Amesema kuwa, Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzania wa vyama, dini na makabila mbalimbali, vilevile anasikiliza malalamiko ya makundi mbalimbali na kuyafanyia kazi akitolea mfano suala la kuruhusu Vyama vyote vya Siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara ili kueleza sera zao na kwamba nia ya Rais ni kujenga mshikamano na umoja nchini.

Kuhusu uchaguzi wa  Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dk Biteko ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi walio bora na kwamba watu wasigawanyike na kufarakana sababu ya uchaguzi, bali waungane katika uchaguzi huo kwa kuzungumza yale yanayowaunganisha kama vile barabara, maji, umeme na wasiruhusu mtu kupandikiza chuki katikati yao.

Amesema hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo itaendelea kuimarika kwani imejengwa njia mpya ya umeme ambayo itapeleka umeme wilayani humo kutokea kituo cha Nyakanazi, pia itajengwa njia nyingine ambayo itapeleka umeme Mbogwe kutokea Kahama na pia kitajengwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wilayani humo kama ambavyo ujenzi wa vituo hivyo utakavyofanyika katika wilaya nyingine nchini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akiwasilisha salam za Mwaka Mpya 2024 alisema anaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Mbogwe ikiwemo miradi ya Elimu, Maji, Umeme, Barabara pamoja na Afya.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Geita, Shigella amesema kuwa, asilimia 90 ya vijiji vya mkoa wa huo tayari vimeshapatiwa umeme na vijiji 50 vilivyosalia kazi za kusambaza umeme zinaendelea ikijumuisha mipango ya kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji.

“Tunamshukuru Rais, Dk Samia amefanya kazi kubwa kuleta fedha  za maendeleo mkoani Geita na tunaahidi kuendelea kusimamia miradi yote ili itekelezwa  kwa wakati. ” Amesema  Shigella.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga, amemshukuru Dk Biteko kwa kufika Mbogwe kushiriki na wananchi pia amempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya nchini na kwa kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo wilayani Mbogwe huku akiongeza kuwa, wanajipanga kuifanya wilaya ya Mbogwe kuwa yenye mabadiliko makubwa ifikapo mwaka 2027.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments