WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kufika katika ofisi za Wakala wa Maji na Usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (Ruwasa) na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Lindi (Luwasa) kufuatilia upungufu uliopo.
Moja ya changamoto ni kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu Juni, mwaka jana ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.
“Hii wizara ina waziri makini, mnafanya vitu kwa ufichouficho. Sasa waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika. Vitu vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwa nini mpo hapa,” alihoji na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.
Alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika ofisi za Ruwasa zilizopo Manispaa ya Lindi jana na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana, huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu amehoji: “Ni kwa nini mtambo huu haujaanza kufanya kazi kwa kipindi cha miezi sita ikiwa katika mikoa mingine imeshaanza kufanya hivyo.
“Mwezi wa sita hadi leo hamjachimba hata kisima kimoja na mnasema kuna matope haiwezekani. Rais ameleta mtambo wananchi wameona gari limefika mnataka visima visichimbwe”?
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na Ruwasa Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili. “Huu ni uzembe, haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi pikipiki zimeanza kuharibika,” alisema.
Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo, Ofisa Manunuzi wa Ruwasa, Kennedy Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao makuu ya Ruwasa bila ya mafanikio.
Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.
Aidha, Majaliwa amechukizwa na hali ya mazingira ya ofisi ya Luwasa ambayo haiendani na ofisi za umma kwani ni machafu na yana vichaka vingi. “Hapa ndio ofisini, kwa hiyo hapa tupo kazini,” alihoji wakati alipokuwa akikagua maeneo hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maji na Msajili wa Hazina wafanye tathmini ya kina kuangalia utendaji kazi wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ambayo ipo ndani ya Ruwasa kuona kama ipo haja ya taasisi hiyo kuendelea kujitegemea.
“Hamuwezi kuwa na wakala mbili zinazofanya kazi moja kwenye taasisi moja,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Lindi, Muhibu Lubasa alisema mkoa umejipanga kuanza kuchimba visima katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa kutumia mtambo huo uliotolewa na Rais Samia kuanzia Februari, mwaka huu.
0 Comments