MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewataka wajasiriamali wa Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo Dodoma na hasa kuzingatia ukuaji wa kasi wa jiji baada ya maamuzi ya serikali kuhamishia shughuli zake zote Dodoma.
Mavunde ameyasema hayo katika viwanja vya Nyerere Square wakati wa zoezi la kugawa majiko na mitungi ya gesi 500 kwa Mama Lishe na Baba Lishe wa Jijini Dodoma.
“Tunaishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa fursa nyingi za kiuchumi zitokanazo na shughuli mbalimbali kufuatia serikali kuhamia Dodoma, ni nafasi ya kipekee ambayo wanadodoma tunapaswa kuichangamkia badala ya kuwa watazamaji wa fursa, “amesema Mavunde
Aidha, ameishukuru kampuni ya ORYX kwa kusaidia upatikanaji wa majiko 500 kwa ajili ya Wanadodoma,ili kupunguza athari za mazingira zitokanazo na matumizi ya mkaa na kuni.
‘Naamini majiko haya yatachochea zaidi shughuli za kiuchumi kwa wajasiriamali na hivyo kuboresha shughuli zao za kipato cha kila siku,” amesema
Amesema, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaandaa utaratibu wa upatikanaji wa mitambo ya kutengeneza mkaa mbadala (briquette) na kugawa kwa vikundi vya wakina mama na vijana.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Charles Mamba wamepongeza zoezi la ugawaji majiko kwa wajasiriamali huku wakisisitiza juu ya elimu ya kutosha ya matumizi ya majiko hayo ili yasilete athari baadaye.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORYX Benoit Araman amesema Kampuni yake inaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi kwa wananchi na kwamba wataendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kutimiza lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi ifikapo mwaka 2032.
0 Comments