Msako kuwakamata wazazi wasiopeleka watoto shule waja Bukoba

KAGERA: Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Bukoba itaanzisha msako wa nyumba kwa nyumba ifikapo Januari 22 mwaka huu kwa ajili ya kuwawajibisha wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka wanafunzi shuleni.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima amefanya ziara katika Kata Kashai na kutoridhishwa na idadi ya wanafunzi waliofika shuleni mpaka sasa kuanza kidato cha kwanza ambapo amechukua nafasi kubwa kuongea na wazazi na walezi juu ya watoto kufika shuleni kwa wakati na namna serikali ilivyoweka nguvu kubwa katika kutafuta ada na kuboresha miundombinu ya elimu.

“Hakuna asiyejua umuhimu wa elimu , Serikali iliondoa kila kitu ada ,madawati na gharama kubwa kwa ajili ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu,lakini pia serikali imeweka nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu,tunachopaswa kufanya sisi ni kuwabeba watoto wetu na kuwapeleka shule sasa tunapowabakisha nyumbani tunakata nini ,hatutavumilia”alisema Siima.

Alisema kutokana na ukubwa wa kata hiyo walipata kujengewa shule mpya na serikali ambayo ilipewa jina la Samia Suluhu na mwaka 2024 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule hiyo ni 98 ikiwa wanafunzi wasichana ni 43 na wavulana ni 55.

Alisema mpaka Januari 11 wanafunzi waliofika shuleni wavulani ni 14 tu na wasichana ni 10 huku idadi kubwa ya wazazi wakiwa hawajafika shuleni kutoa taarifa za watoto wao juu ya kuchelewa kufika shuleni .

Alisema kuwa shule ya Sekondari ya Kashai ilichagua watoto 550 wa kuripoti kidato cha kwanza ikiwa wasichana ni 250 na wavulana 250.

Alisema mpaka Januari 11 wavulana waliofika shuleni kuanza kidato cha kwanza ni 148 na wasichana ni 157 sawa na asilimia 54 ya wanafunzi wanaopaswa kuwa shuleni .

Alisema kuwa serikali haitawafumbia macho wazazi na walezi ambao hawataonyesha nia ya kuwapeleka watoto shuleni huku akiwahakikishia wazazi kuwa hakuna huduma za ziada katika kumpeleka mtoto shule hivyo wafanye haraka kabla ya msako huo kuwafikia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments