TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa tumbaku kwa mwaka 2022/2023.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa X na kuongeza kuwa uzalishaji wa zao hilo nchini umeongezeka kutoka tani 50,000 hadi tani 122,858 mwaka 2023/2024.
Aidha amesema hadi kufikia Desemba mwaka jana, thamani ya mauzo ya tumbaku ilikuwa Dola milioni 316 kuelekea lengo la kufikia Dola milioni 400.
Waziri Bashe alibainisha kuwa kwa msimu wa 2024/2025 wanatarajia kufikia tani 200,000 ambapo malengo ni 300,000 ifikapo 2025/26.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Zimbabwe inaongoza kwa kuzalisha tani 296,000, ikifuatiwa na Tanzania, Malawi (tani 121,000), Msumbiji (tani 65,800), Zambia (tani 44,000) na Uganda (tani 13,000) katika orodha hiyo.
Aliendelea kwa kuvipongeza vyama vya wakulima pamoja na kampuni za tumbaku nchini akieleza kuwa kwa mara ya kwanza zaidi ya asilimia 50 ya tumbaku imenunuliwa na kuuzwa nje ya nchi kwa asilimia 100 na makampuni ya ndani.
“Haikuwa safari rahisi. Nawashukuru wafanyakazi wote wa bodi ya tumbaku, tuliota na tumetekeleza. Tutakuwa mzalishaji namba 1 barani Afrika.” waziri alisema.
0 Comments