Wadau wataka wagombea urais wachukuliwe fomu

WADAU wameendelea kutoa maoni mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu miswada ya uchaguzi na kushauri kuwa mgombea wa urais anaweza kuchukuliwa fomu ya kuteuliwa na chama au wakala.

Jana ni siku ya tatu kwa kamati hiyo kupokea maoni kwa ajili ya marekebisho ya sheria nne ambazo ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Akitoa maoni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda alisema CCM inakubaliana na mapendekezo ya vifungu vilivyowasilishwa katika miswada kwa nia ya kuboresha na kuwa moja ya eneo jipya, katika muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kuanzishwa kwa sharti lenye kumtaka mgombea mwenyewe kuchukua na kurejesha fomu ya uteuzi.

“Hii inashauriwa kwamba sharti hilo lirekebishwe na badala yake chama au wakala wa mgombea aruhusiwe kumchukulia mgombea wake isipokuwa fomu hiyo ni lazima irejeshwe na mgombea mwenyewe,” alisema.

Alisema pia utaratibu uliotumika wa kuzichukua ibara za Katiba kama zilivyoainishwa na kuziingiza katika miswada ya sheria hiyo ni njia sahihi ya kuhakikisha kwamba sheria hizo hazipingani na Katiba ya nchi, hivyo utaratibu huu uendelee kuzingatiwa.

Chatanda alisema muda unaopendekezwa katika muswada wa sheria kwa Tume ya Uchaguzi kukutana mara nne kwa mwaka na wakati wowote inapohitajika ni muhimu eneo hilo na kupendekeza kuwa hilo liangaliwe upya ili kupunguza gharama za uendeshaji wa chombo hicho.

Alisema kwa kuwa taifa linakabiliwa na changamoto ya wapigakura kushindwa kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura zao siku ya uchaguzi, changamoto hiyo mpaka sasa bado haijapatiwa ufumbuzi wa kisheria, ni muhimu kwa muswada wa sheria ya Tume ya Uchaguzi kuanzisha idara au kitengo mahususi katika muundo wa tume ya taifa ambacho kitakuwa na jukumu ya kutoa elimu ya mpigakura.

Chatanda alisema ingawa Mahakama imeruhusu wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji kuwa wasimamizi wa uchaguzi hata hivyo inapendekezwa kwamba watendaji hao sio lazima kwa sheria kuwataja waziwazi.

Alisema moja ya sharti jipya linaloanzishwa chini ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ni kukitaka chama cha siasa chenye usajili kamili kuweka kwenye katiba yake kifungu kinachoelekeza kuwa na sera ya jinsia na ujumuishi na makundi maalumu, hivyo CCM inapendekeza kifungu hicho kiboreshwe zaidi kwa kuongeza sharti la kikatiba chama cha siasa chenye usajili kamili kuweka katika katiba yake kifungu chenye kuainisha itikadi yake.

Chatanda alisema muda wa siku 30 unaopendekezwa wa chama cha siasa kuwasilisha ripoti ya marejesho ya gharama za uchaguzi katika chaguzi ndogo ni mchache, uongeze hadi kufikia siku 60.

Naye Askofu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania na Askofu mstaafu wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Pentekoste Tanzania (CPCT), Peter Konki alipendekeza kuwa uteuzi wa wakurugenzi wa uchaguzi kuendelea kuteuliwa kutoka miongoni mwa watumishi wa umma ambao ni wigo mpana unaojumuisha ofisi zote zinazohusiana na umma vikiwemo vyama vya siasa.

Pia alipendekeza kuwa Mwenyekiti na Makamu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wasipitie katika taratibu za usaili badala yake waendelee kuteuliwa kwa mujibu wa katiba.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Mkuu, Dk Fredrick Shoo amempongeza Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kufanya maboresho ya sheria ambazo zitaunganisha taifa.

Akitoa mapendekezo ya CCT, Mwanasheria, Gloria Mafole alipendekeza kuwa uandikishaji mawakala uongezeke kutoka siku saba hadi 14 kwa kuwa muda uliowekwa katika muswada huo ni mfupi.

Happines Mamuya ameshauri Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Ubunge na Udiwani kuna umuhimu wa kuweka utaratibu kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) kupigakura kwa njia ya mitandao au katika ofisi za balozi za Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini alishauri kuundwa kwa kifungu kipya katika muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi ambacho kitawalinda wakurugenzi wa uchaguzi, kama wanavyolindwa majaji.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Joseph Mhagama alisema Kamati haitafanyia kazi maoni ambayo yanakwenda kinyume na katiba.

VIDEO: MSIACHE KUTUMIA OFISI ZETU KWA MSAADA WA KISHERIA

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments