KIGOMA: Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye ametaka watendaji wa serikali mkoani humo kutumia vitendea kazi vinavyotolewa na serikali ikiwemo magari yatumike kufikia malengo ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Amesema magari hayo yawe tija badala kutumika kuzunguka nayo kwenye maeneo ya starehe.
Andengenye amesema hayo akikabidhi magari saba aina ya Toyota Hard Top yatakayotumika kwa ajili ya mpango wa usimamizi shirikishi wa sekta ya afya unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi ili kutoa huduma za uhakika na za kuaminika.
Magari hayo saba yanaufanya Mkoa wa Kigoma kupokea jumla ya magari 15 ambapo awali yaliyotolewa magari nane ya kubebea wagonjwa (Ambulance) yaliyotolewa na Raisi Samia Suluhu Hassan katika mpango wake wa kuboresha sekta ya afya nchini.
Awali Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Albert Msovela alisema kuwa magari hayo yatakwenda kwenye mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya usimamizi kwenye sekta ya afya ikiwemo ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RMO), Hospitali ya rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni, Halmashauri ya wilaya Buhigwe, Kibondo, Kasulu Mji, Halmashauri ya wilaya Uvinza na Chuo cha Waganga Maweni mjini Kigoma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk. Jesca Leba alisema kuwa tayari ofisi yake imeshapokea magari manane ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ambayo yameshapelekwa kwenye vituo vilivyolengwa na yameanza kutoa huduma na kwamba magari haya saba ya awamu ya pili yatawasaidia katika kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za afya mkoani humo.
0 Comments