Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA ameagiza Malori yote yanayopaki kwenye Stendi ya Mabasi wilayani Manyoni kuondolewa ili kuleta usalama kwa abiria na watumiaji wengine wa Stendi hiyo.
MLATA alitoa agizo hilo wakati akiwa katika Ziara yake ya kukagua Miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa serikali kupitia Ilani ya CCM wilayani Manyoni.
Alisema sio jambo jema kwa Mabasi na Malori kupaki katika Stendi hiyo ambayo ilitengwa kwa ajili ya mabasi tu.
Baadhi ya watumiaji wa Stendi hiyo walisema usalama katika Stendi hiyo umekuwa mdogo kutokana na Mabasi, Malori mizigo na mafuta kupaki kwa pamoja katika Stendi hiyo.
Waliongeza kuwa kutokana na Malori hayo kupaki kwenye Stendi hiyo imesababisha baadhi ya Mabasi kupitiliza bila kuingia ndani ya Stendi na wakati mwingien kushusha abiria nje ya Stendi.
Hata hivyo wameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto hiyo ya Malori ambayo pia yamekuwa yakiiharibu Stendi hiyo kutokana na uzito wa mizigo yanayobeba.
Kwa upande wake uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni walisema wanaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wanatenga eneo jingine ambalo Malori hayo yatakuwa yanapaki.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida ilitembelea Kituo cha Afya Kata ya Sanza, ambapo baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo waliishukuru serikali kwa kuendelea kutekeleza Miradi ambayo inawaondolea adhaa wananchi ya kufuata huduma za Afya na kijamii umbali mrefu.
0 Comments