CCM wasitisha ziara maombolezo kifo cha Lowassa

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesimamisha ziare yake ya mikoa 20 na kuungana na Wanachama na Watanzania wote katika siku tano za maombolezo ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowasa aliyefariki Februari 10, Mwaka huu.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Ruvuma.

“Tumeona ni vyema tuhairishe ziara katika mikoa miwili iliyobaki ili tuungane na Watanzania wote katika kipindi hiki cha maombolezo na sisi kama Chama Cha Mapinduzi ambacho amekitumikia kwa miaka mingi tangu akiwa kijana, hadi nafasi ya juu kabisa,”

“Ni busara na tuwaombe wananchi katika mikoa iliyobaki ya Mtwara na Lindi kwamba ziara yetu tutaipanga tena kwa wakati mwingine ili sasa tuungane na Watanzania wote katika maombolezo haya ya siku 5,” alisema Makonda.

Makonda alitoa wito kwa Watanzania wote kwa ujumla kuungana na familia na Ndugu wa Marehemu katika kuwaombea katika kipindi hiki kigumu cha majonzi wanachopitia.

“WanaCCM kokote walipo na wapenzi wa Chama chetu katika Mkoa wa Arusha, Dar es Salaam na maeneo mengine pale ambapo familia itakapotupa ratiba na viongozi wetu wakuu wakitutamkia cha kufanya basi tushirikiane kwa pamoja, zipo shughuli mbalimbali ambazo Chama tungefurahi kuona tunazifanya katika namna ya kumuenzi na kutambua mchango wake kuhakikisha kwamba kila kinachotakiwa kufanywa kifanyike,” alisema.

Pia alitoa rai kwa Viongozi wengine wa vyama mbalimbali vya siasa nchini kuachana na shughuli zingine zote za kisiasa na kuungana katika maombolezo ya msiba huu mzito wa Taifa.

“Nafahamu kwamba kuna shughuli mbalimbali zinaendelea za kisiasa, tunawaomba kwakuwa serikali yetu na Chama chetu kina shiriki mambo mengi ya kitaifa na kwakuwa Mzee wetu Edward Lowassa amekuwa kiongozi na amegusa watu wengi,”

“Na wao pia watani zetu watafahamu mchango wake katika Chama hivyo tuungane katika hili, tusitishe shughuli zote za kisiasa, tuungane katika maombolezo haya ya siku 5 yaliyotangazwa na Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa Chama na kuhakikisha tunamuhifadhi katika nyumba yake ya milele kiongozi wetu kwa heshima zote ananzostahili,” alisema.

Makonda aliongeza kuwa ratiba ya muendelezo wa ziara itatolewa baada ya kumalizika kwa maombolezo hayo.

“Ratiba tutaitoa wakati mwingine ili tuweze kuimalizia ziara katika mikoa iliyokuwa imebaki, dhamira yetu ni kuendelea kuwatumikia watanzania na kuyagusa makundi yote katika nchi yetu na kuwaheshimu viongozi wetu ambao wanaofanya kazi katika Taifa hili ndani ya Chama chetu na ndani ya serikali yetu,”
alisema.

Aidha Makonda aliwashukuru wenyeviti na makatibu wote wa CCM kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi kata kwa ushirikiano walionyesha wakati akizunguka katika ziara hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments