DC Bariadi ataka jimbo kugawanywa

SIMIYU: Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga amesema,  wilaya hiyo inalo Jimbo moja la Bariadi, ambalo ameeleza linatakiwa kugawanywa na yawe majimbo mawili ili kuweza kuletea maendeleo ya haraka wananchi wananchi wa wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa jimbo hilo linavyo vigezo vyote vya kugawanywa, ambapo kigezo cha kwanza ni wingi wa watu kwani kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2022 jimbo hilo lina jumla ya watu 644, 312.

Simalenga ametoa kauli hiyo leo wakati wa mafunzo ya matokeo ya sensa ya watu na makazi 2022, yaliyoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema kuwa moja ya vigezo vinavyounda jimbo ni idadi ya watu, na kanuni zinataka jimbo moja la uchaguzi lisiwe na watu zaidi ya Laki nne (400,000), ambapo Jimbo la Bariadi limezidi idadi hiyo.

Mbali na hilo Simalenga amesema kuwa katika sheria hizo, zinataka jimbo lisiwe na halmashauri zaidi ya moja, ambapo Jimbo la Bariadi linazo halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji na Bariadi Vijijini.

Amesema kuwa kwa vigezo hivyo, Jimbo la Bariadi linatakiwa kugawanywa ili kuweza kurahisisha shughuli za maendeleo kuweza kuwafikia wananchi wake kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wale wote wanaopinga kugawanywa kwa jimbo hilo, kutanguliza maslai mapana ya wananchi wa wilaya hiyo pamoja na kusukumwa na utashi wa maendeleo kwa wananchi wao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments