MAKAMU WA RAIS AWASHA UMEME WA REA KATIKA KITUO CHA AFYA KETUMBEINE

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango amewasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine, kilichopo katika kijiji cha Armanie wilayani Longido, Mkoa wa Arusha na kupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusambaza nishati hiyo kwa ufanisi.


Akizungumza leo Februari 10, 2024 na umati wa wananchi katika uwanja wa Kituo cha Afya Ketumbeine baada ya kuwasha umeme na kukizindua rasmi, Dkt. Mpango amesema azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwapelekea wananchi maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na Serikali anayoiongoza.

“Nimefika hapa, kwanza tumewasha umeme kwa ajili ya kituo hiki cha Afya. Napenda niwapongeze sana watu wa REA kwa kazi nzuri. Sasa Kituo chetu cha Afya, nina hakika wananchi watakaokuja kupata huduma hapa watapata huduma ya uhakika,” amesema.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Arusha, mbele ya Makamu wa Rais, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa Serikali kupitia REA imewekeza jumla ya shilingi Bilioni 73.9 kwa Mkoa huo.

Amesema fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi mitano ya umeme vijijini ambapo jumla ya vijiji 263 kati ya 268 vya Mkoa wa Arusha vimekwishafikishiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, ikiwa ni asilimia 71.46.

Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, vijiji vilivyosalia vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA na kwamba ifikapo Juni mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimekwishafikiwa.

Ameitaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na REA mkoani Arusha kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Akifafanua zaidi, amesema kuhusu Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, fungu la Kwanza limekamilishwa kwa asilimia 61 likihusisha uwashwaji wa vijiji 27 kati ya 44; na la Pili limekamilika kwa asilimia 95 likihusisha uwashwaji wa vijiji 58 kati ya 61.

Akizungumzia malengo ya kutekeleza Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa unalenga kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha ambapo wigo wa kazi unahusisha kuyafikishia umeme maeneo 81 kwa gharama ya shilingi Bilioni 11.

Kwa upande wa Mradi wa kupeleka umeme katika Migodi midogo na maeneo ya kilimo, wigo wa kazi unalenga kuifikia migodi na maeneo ya kilimo 27 kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.5.

Aidha, Mhandisi Saidy amesema kuwa Mradi wa kupeleka umeme katika Taasisi za Afya na Pampu za Maji unalenga kupeleka umeme katika maeneo hayo ambayo hayajafikiwa ili kupambana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo UVIKO-19.

“Wigo wa kazi unahusisha kupeleka umeme katika pampu za maji 17 kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.5 na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 9 ambapo kazi ya ujenzi imefikia asilimia 97.”

Tukio la kuwasha umeme na kuzindua Kituo cha Afya limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Maafisa wa Serikali pamoja na wananchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akibonyeza kitufe  kuashiria kuwasha umeme kwa mara ya kwanza kwenye Kituo cha Afya cha Ketumbeine kilichopo katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, leo tarehe 10 Februari, 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa kwanza kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi, Hassan Saidy (mwenye fulana ya njano) pamoja na Viongozi wengine mbalimbali alipowasili katika hafla ya kuwasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo katika kijiji cha Armanie, wilayani Longido Mkoa wa Arusha leo tarehe 10 Februari, 2024. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Uhamasishaji Rasimali kutoka REA, CPA Daniel Mungure.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea taarifa ya miradi ya nishati vijijini kwa Mkoa wa Arusha kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi Hassan Saidy wakati wa Hafla ya kuwasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie wilayani Longido Mkoa wa Arusha, leo Februari 10, 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akikata utepe kuzindua kituo cha afya Ketumbeine katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie wilayani Longido, Mkoa wa Arusha. Kituo hicho kimeunganishwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Tukio hilo limefanyika leo Februari 10, 2024
Kutoka kulia ni Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy na Viongozi wengine wa Serikali wakifuatilia hafla ya kuwasha umeme na kuzindua Kituo cha Afya Ketumbeine, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, leo Februari 10, 2024. Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

Sehemu ya umati wa wananchi walioshiriki kwenye hafla ya kuwasha umeme na kuzindua Kituo cha Afya Ketumbeine katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie wilayani Longido, Mkoa wa Arusha. Kituo hicho kimeunganishiwa  umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika leo Februari 10, 2024 alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Taswira ya Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie, Wilaya ya Longido mkoani Arusha. Taswira hii ilichukuliwa leo Februari 10, 2024 muda mfupi kabla Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Philip Mpango kuwasha umeme uliofikishwa kituoni hapo kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments