Makonda Awavaa Wafanyabiashara Wanaoipenda CCM Kwa Kubipu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda amewashukia baadhi ya wafanyabiashara nchini akisema wanaigiza kukipenda chama hicho kwasababu ya kulinda biashara zao.

Akihutubia wakazi wa mjini Iringa na vitongoji vyake katika mkutano mkubwa wa hadhara unaoingia katika kumbukumbu ya mikutano ya chama hicho iliyovuta watu wengi zaidi mjini Iringa, Makonda alisema:

“Wafanyabiashara wengi nchini wanaichangia CCM sio kwasababu wanaipenda ni kwasababu wana hofu isiyo na uhalisia wowote kwamba kwa kuwa ni chama dola kinaweza kuitumia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) au Polisi kudhibiti biashara zao.

Alisema serikali ya CCM inafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na kuwataka wafanyabiashara hao waondoe hofu hiyo.

“Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wafanyabiashara hao wanakuwa sehemu ya chama hicho, wakipende, wakipiganie na wafanye kazi zake kwa upendo wa dhati,” alisema.

Amewataka wana CCM kuanzia ngazi ya shina na kuendelea kuacha unyonge na kuwa rufaa ya kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

“Chama hiki ndicho kilichounda serikali. Tunataka mwananchiasipohudumiwa vizuri katika mamlaka za serikali akimbilie kwenye chama, chama kiwe rufaa ya kero za watu zinazocheleweshwa au kushindwa kabisa kushughulikiwa,” alisema.

Kuhusu matokeo ya fedha zinazotolewa na serikali kusukuma maendeleo ya nchini, Makonda alisema taarifa za umma sio siri za viongozi na kwamba wanaozificha wanawachanganya wananchi.

“Viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa katika ngazi zote mna wajibuwa kimsingi wa kueleza kwa umma mipango na kazi zinazofanywa na serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan badala ya kusubiri viongozi wa juu waifanye kazi hiyo.

Alisema imekuwa ni kawaida kwa viongozi wengi hususani katika ngazi ya mtaa hadi mkoa kuzikalia kimya taarifa mbalimbali nzuri za serikali jambo linalowafanya wananchi wengi wasiwe na ufahamu wa mambo wanayopaswa kuyajua kuhusu serikali yao.

“Viongozi hao ndio vinara wa kauli ya mama ameleta mabilioni. Nakereka sana na kauli hiyo kwasababu viongozi hao ni wavivu kuwataarifu au kuwaonesha wananchi namna mabilioni hayo yalivyotumika kujenga au kuboresha huduma zinazowahusu,” alisema.

Makonda alizungumzia vitendo vya rushwa, ufisadi na kero mbalimbali zinazodhohofisha maendeleo ya nchi na wananchi kwa kuomba dua na sala za viongozi wa dini zisiishie kuwaombea viongozi wa juu wa serikali peke yao.

“Kwa kuwateteta wanyonge wan chi hii, tunachukiwa na mafisadi, wale rushwa na waovu wa kila aina. Kusaidia kumaliza changamoto hii, viongozi wa dini waombeeni watu wote waliobeba dhamana ya kushughulikia changamoto za watu watende haki,” alisema.

Alisema watu wanaounda serikali ya CCM sio malaika wala hawajatoka mbinguni kuja kutekeleza majukumu waliyopewa, ni watanzania kama walivyo wengine, kama hawatendi haki, wanyonge wataendelea kuumia na kulia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments