MIRADI YA MAENDELEO MKOANI SINGIDA NI MKOMBOZI KWA WANANCHI

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA amesema fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali zipo salama na zinasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija kwa wananchi.

Mlata alisema hayo katika Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni katika ziara ya kamati ya siasa Mkoa wa Singida, ambapo alisema viongozi wa Chama na Serikali wanashirikiana kuzisimamia fedha hizo.

Alisema Wananchi wanafurahi kuona fedha hizo zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza Miradi katika maeneo yao.

Aidha aliridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji katika kijiji cha Mabondeni, ambao unatarajia kuwaondolea adha wananchi ya kufuata Maji umbali mrefu.

Hata hivyo amemtaka msimamizi wa Mradi huo, kuukamilisha kwa wakati ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake MNEC wa mkoa wa Singida YOHANA MSITA aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi kwa kutekeleza Miradi mbalimbali.

Alisema Mradi huo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Mabondeni pale utakapoanza kutoa huduma ya maji.

MSITA pia alitoa wito kwa TANESCO kuhakikisha wanaharakisha kupeleka umeme kwenye chanzo hicho cha maji ili isije kutokea Mradi unakamilika halafu ukakwamishwa na kukosekana kwa umeme.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida BERTHA NAKOMOLWA aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo katika miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi huo wa Maji CHRISTOPHER NDAHANI aliahidi Mradi huo kuwa utakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Mabondeni.

                  


                         








TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments