BAADHI ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa nchini wameguswa kwa namna yao kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa aliyefariki leo akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Baada ya Rais Samia, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu kutoa pole zao kufuatia kifo cha kiongozi huyo, baadhi ya viongozi akiwemo Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba pia ametoa pole yake.
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa X Mwigulu ameandika: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Mzee wetu Edward Ngoyai Lowassa. Tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa aliotoa kwa Maendeleo ya Taifa letu”.
Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye pia kupitia mtandao huo ameandika: “Nape, tumepishana kwenye siasa, lakini napenda mtu anayesimamia anachoamini hasa kwa umri wenu” Haya yalikuwa maneno ya Edward Lowassa tulipokutana mara tu baada ya uchaguzi wa 2015! Pumzika kwa amani kiongozi”.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo naye kwenye mtandao wa X ameandika ujumbe wake unaosomeka: Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa, natoa pole kwa Familia na Watanzania wote kwa kuondokewa na Kiongozi wetu aliyewahi kuhudumu nafasi mbalimbali katika siasa na Serikali ya JMT. Apumzike kwa amani”.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe pia ni miongoni mwa walioguswa na kifo cha Lowassa ambapo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X ameandika: Nimesikitishwa sana kusikia msiba wa Mzee Edward Ngoyai Lowasa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Salaam zangu za rambirambi ziwe pamoja na familia yake wakati huu mgumu kwao. Mungu awape nguvu na mshikamano wa dhati. Poleni wana Monduli na Arusha.”
0 Comments