JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi maeneo ya Mji Mwema, Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwanywesha dawa inayodhaniwa kuwa ni sumu na kuwalewesha watu 16 wa familia moja na baadaye kuwaibia simu.
Taarifa iliyotolewa leo Februari 20, 2024 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, ACP Muliro Jumanne Muliro imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Februari 18, 2024 kuanzia 3:00 usiku ambapo mtu huyo aliyejifanya mganga wa jadi alipofika nyumbani kwa familia ya Halisi Amani kwa lengo la kumtibia mke wake Fatuma Abdalla (52) aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo la miguu.
Aliwanywesha dawa iliyowalewesha familia nzima, wakapoteza fahamu na akawaibia simu tano za mkononi na kuondoka.
Aidha, kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtafuta mganga huyo pia limemkamata kwa mahojiano mtu mmoja anayefamika kwa jina la Jalala Ally Said anayedaiwa kushirikiana na mganga huyo.
Pia amesema wagojwa walilazwa na kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni mpaka sasa wagonjwa 13 wamesharuhusiwa na wengine watatu waneendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Tukio lingine limetokea Februari 9, 2024 eneo la Tuangoma, Mbagala ambapo mtu mmoja aliyejifanya mganga wa jadi aliwanywesha dawa zilizowalevya na baadae kupoteza fahamu watu watano na kuwaibia pikipiki namba MC474, simu 3 za mkononi na Sh 30,000.
Jeshi la polisi linawatahadharisha wananchi kuhusiana na kuwepo kwa watu wanaojifanya waganga wa jadi ambao huwalewesha watu na wanafamilia kwa ujumla na baadae kuwaibia.
0 Comments