Rais Samia Awaita Poland Kuwekeza Tanzania

DAR ES SALAAM: Rais Samia Suluhu Hassan amesema timu ya wataalam imeshaelekezwa kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za moja kwa moja kati ya Poland na Tanzania.

Aidha, Rais Samia amesema safari hizo zitachochea zaidi utalii pamoja na biashara kwa kuwa Poland ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kuwa na watalii wengi nchini.

Rais Samia amesema hayo leo Ikulu akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku 2 wakati wakizungumza na vyombo vya habari.

Vile vile, Rais Samia amewakaribisha wawekezaji kutoka Poland kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta ya utalii hususan ujenzi wa hoteli.

Rais Samia pia amesema Tanzania na Poland zitaendelea kushirikiana katika sekta za elimu na kuhamasisha uwekezaji zaidi kwenye sekta za kimkakati kama vile viwanda, uzalishaji, nishati, madini, gesi asilia na uchumi wa buluu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Poland ipo tayari kutoa bima kwa benki za biashara kupitia Wakala wa Mikopo ya Usafirishaji kwa ajili ya kutekeleza mradi wa reli ya kisasa kwa vipande vya Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka.

Poland ni nchi yenye uchumi wa 21 kwa ukubwa duniani hivyo ziara ya Rais Duda inatoa fursa kwa Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kimkakati ambazo imedhamiria kuimarisha mahusiano ya kiuchumi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments