DODOMA: Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza mazungumzo na Kampuni ya TAQWA-DALBIT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na maeneo yenye wachimbaji wadogo ili kuchochea shughuli za uchimbaji madini nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Naibu Waziri Madini Dk Steven Kiruswa pamoja na Menejimenti ya Uongozi wa Kampuni ya TAQA-DALBIT ikiongozwa na Meneja Mkuu Amr Aboushad na Mkurugenzi wa maendeleo ya Biashara Raphael Banzi
Akiwasilisha maelezo ya awali, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Amr Aboushad amesema wapo tayari kuzalisha umeme kupitia gesi kwa kufunga mtambo katika migodi na maeneo ya wachimbaji.
Amesema kufungwa kwa mitambo hiyo kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya nusu ya gharama inayotumika hivi sasa kupitia matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli.
Amesema pia itahusisha uzalishaji wa umeme kupitia mfumo wa umeme jua ambapo Kampuni itafunga mtambo mkubwa kwa gharama yao na kuwaunganisha wachimbaji wadogo kwa malipo ya mwezi ya matumizi ya nishati hiyo.
Nae, Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza ameishukuru Kampuni kampuni hiyo kwa utayari wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na kuagiza uongozi wa Wizara kuitisha mkutano wa haraka na wadau wote wakiwemo wachimbaji wadogo na wakubwa ili kupata fursa ya kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa mpango huu
0 Comments