Tanzania, Urusi kuenzi miaka 62 ya ushirikiano

DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema kuwa CCM, chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kudumisha uhusiano na urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, ukilenga kuboresha maeneo ya uwekezaji, biashara na uchumi, kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.

Balozi Dk Nchimbi amesema hayo leo Februari 22,2024 ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, ambapo amesisitiza kuwa kuboresha maeneo ya uwekezaji, biashara na uchumi, kutaimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali za nchi hizo mbili na wananchi wake na kuufanya kuwa wa moja kwa moja zaidi.

Akirejelea kumbukumbu za uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Urusi, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambao mwaka huu unafikisha miaka 62, walizungumzia maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa kazi na Serikali za nchi hizo, chini ya uongozi wa vyama vinavyoongoza nchi hizo, Chama Cha Mapinduzi na United Russia, mtawalia.

Kwa upande wake, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, mbali ya kumpongeza na kumtakia kila la heri Balozi Dk. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, ameelezea uhusiano wa muda mrefu wa Urusi kwa Tanzania na nchi za Afrika, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambapo ilikuwa mojawapo ya nchi za mwanzo kuitambua Tanganyika huru, akisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Vladimir Vladimirovich Putin, na mazingira mazuri ya uwekezaji, biashara na uchumi ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Urusi iko tayari kuendelea kuenzi na kuimarisha uhusiano utakaonufaisha pande zote mbili.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments