Katibu Mkuu wa wizara ya Afya Dkt John Jingu amewataka Waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanasimamia na kuimarisha mawasiliano baina ya mtoa huduma na mpewa huduma kwa kuzingatia matumizi ya lugha zenye staha.
Dkt. Jingu ameyasema hayo Leo Februari 14, 2024 Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa mwaka wa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi, ambapo amesisitiza wapo baadhi ya watoa huduma wanaharibu taaluma hiyo kutokana na kukosa namna sahihi za kuwa wakarimu kwa wagonjwa jambo linalopekea Manung'uniko makubwa katika jamii.
"Baadhi yetu, kunachangamoto kubwa ya lugha wanazozitumia wakati wa kutoa huduma kwa wahudumiwa si za staha na hii inaleta malalamiko, wakati mwingine tunalazimka kuunda timu, tunapoteza rasilimali baada ya kupeleka fedha katika kuboresha huduma tunaanza kuchunguzana, lugha ya staha ni muhimu ukizingatia tunaowahudumia ni wagonjwa ni watu wenye shida." amesema Dkt. Jingu.
Pia Dkt. Jingu amelaani vitendo vya baadhi ya watoa huduma za afya nchini kuendekeza matumizi ya simu hasa wawapo katika maeneo ya kazi.
"Hili ni jipya halikuwepo zamani, Unakuta Mgonjwa yupo pale badala ya kumuhudumia mhudumu yupo busy na simu na mgonjwa anaweza pata madhara ambayo kama ungekuwa makini akili yako isingekuwa kwenye simu ungeweza kumsaidia, kwahiyo hili ni jambo ambayo ni lazima tulidhibiti wakati wa kutoa huduma." Amesema Dkt. Jingu
Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kurekebishana kimaadili na uadilifu kwa baadhi ya watoa huduma hasa kudhibiti matumizi mabaya ya miundombinu ya vituo vya afya pamoja na kudhibiti wizi wa Dawa.
"Sisi wote tunaapa kabla ya kuruhusiwa kufanya majukumu yetu, twendeni tukaishi viapo vyetu, na mjue kwamba nyie ndio sekta, tuna mawaziri wetu na sisi wasaidizi wao lakini sekta hasa ni ninyi, 99% ya sekta inapatikana kwenu nyie, twendeni tukailinde sekta yetu watu wapate huduma bora, nyie wote ni wawakilishi wa serikali katika sekta ya Afya bila kujali umiliki ni wanani" amesema Dkt. Jingu
0 Comments