"WANANCHI CHAGUENI VIONGOZI WANAOTOKANA NA CCM, WATATUE CHANGAMOTO ZENU". Spika Zanzibar.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ZUBEIR ALI MAULID amewataka Wananchi wa Mkoa wa Singida kuhakikisha wanashiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kikamilifu na kuchagua Viongozi wanaotokana na Chama cha Mapinduzi - CCM, watakaowasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

ZUBEIR ALI MAULID ambaye pia ni Mlezi wa Chama cha Mapinduzi - CCM Mkoa wa Singida alisema hayo Mkoani Singida wakati akizungumza na Wananchi na Wanachama wa CCM Mkoa huo katika Maadhimisho ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM kimikoa.

Alisema kuwa Chama ni lazima kihakikishe ngazi zote za Uongozi kinashinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

MAULID aliongeza kuwa endapo watafanya vizuri katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa itakuwa rahisi kwao kushinda tena katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Aidha alitoa wito kwa Serikali ya Mkoa na Chama cha CCM Mkoa kuhakikisha wanaendelea kusimamia Miradi yote inayotekelezwa kupitia Ilani ya CCM inakamilika kwa wakati.

Hata hivyo alisema kupitia Maadhimisho hayo ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM watanzania waendelee kudumisha Amani iliyoasisiwa na Viongozi wetu, kwani kuna madai wengi wanaichukia CCM kutokana na Uimara na Umadhubuti wake katika kusimamia Amani, Upendo na Mshikamano nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA alisema ushirikiano kati ya Chama na Serikali mkoani humo ni mzuri.

Alisema Chama na Serikali wameendelea kushirikiana kuhakikisha ILANI ya CCM inatekelezwa kikamilifu ili Wananchi waweze kupata huduma stahiki.

Naye MNEC wa Mkoa wa Singida YOHANA MSITA alisema katika Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Singida umejipanga kushinda ngazi zote za Uongozi kuanzia Vitongoji hadi Vijiji.

Kabla ya kuzungumza na Wananchi wa Singida, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ZUBEIR ALI MAULID ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Singida na Manyara alitembelea na kukagua Miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kupitia ILANI ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida.

Katika Miradi hiyo aliyotembelea na kukagua aliridhishwa na hatua ya Miradi hiyo na ile iliyokamilika, ambapo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais SAMIA SULUHU HASSAN kwa kutekeleza Miradi hiyo ambayo imetatua changamoto nyingi kwa Wananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA akiwa na vijana wa hamasa mkoa wa singida wakisherekea maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ZUBEIR ALI MAULID akikata KEKI ya Kutimiza miaka 47 ya kuzaliwa kwa (CCM) mkoani Singida.Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ZUBEIR ALI MAULID akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Singida katika Maadhimisho ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM kimkoa, yaliyofanyika Manispaa ya Singida.

Na Lafulu Kinala Singida

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments