“Hatujaridhika na urejeshaji fedha za mikopo ya KKK”

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imesema haijaridhishwa na urejeshaji mikopo ya fedha za mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) unaofanyika katika halmashauri mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mzava amesema hayo leo katika ziara ya kukagua utekelezaji mradi huo eneo la Msolwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani na kueleza kuwa mbali na kamati yake kuridhishwa na mradi wa KKK, lakini hawajaridhishwa na namna mikopo hiyo inavyorejeshwa na halmashauri.

Mzava amesema pamoja na halmashauri hiyo kukopeshwa Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa KKK lakini imeshindwa kurejesha fedha kwa wakati.

‘’Kama Kamati bado hatujaridhishwa kabisa namna ya kasi ya urejeshaji fedha hizi na wito na msisitizo wetu zifanyike kila aina ya jitihada kuhakikisha fedha zinarudi ili zikasaidie maeneo mengine yenye uhitaji ili dhamira ya Rais ya kutoa fedha hizo iweze kufikiwa,’’ alisema Mzava

Kwa mujibu wa Mzava, hadi Machi 2024 kwa ujumla wizara imepokea marejesho ya Sh bilioni 22.7 kati ya Sh bilioni 50 sawa na asilimia 45 kutoka kwenye halmashauri na taasisi mbalimbali zilizonufaika na mkopo huo.

Amesema, fedha zinazotolewea kama mkopo usio na riba kwa halmashauri zikirejeshwa zitasaidia kukopesha halmashauri nyingine na hivyo kuisaidia kutatua changamoto za sekta ya ardhi nchini na kuboresha katika maeneo mengine.

Hata hivyo, ametaka kufanyika jitihada mbalimbali ili kusaidia katika urejeshaji mikopo hiyo na kuweza kuzisaidia halmashauri nyingine ili ziweze kuondoa changamoto za sekta ya ardhi nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amebainisha kuwa, mpaka sasa halmashaurii zilizorejesha kiasi chote cha fedha ya mkopo ni 12 huku zile zilizorejesha sehemu ya fedha zikiwa ni 43.

Pinda amesema Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) ni program ya miaka 10 inayotekelezwa na wizara yake kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa programu hiyo ulianza mwaka 2018/2019 na unatarajiwa kukamilika 2028/2029.

Programu hiyo inatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na halmashauri ambazo ni mamlaka za upangaji na sekta binafsi ambapo program hiyo inagharamiwa na serikali kupitia fedha za ndani za bajeti ya maendeleo.

Serikali ilitoa mtaji wa Sh bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa program ya KKK kwa utaratibu wa kuzikopesha halmashauri na taasisi ambapo wizara kwa kushirikiana na wizara ya fedha na Ofisi ya Rais TAMISEMI ziliweka utaratibu kwa kuweka vigezo vya kutoa mkopo huo bila riba kwa ajili ya utekelezaji wa program.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments