KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA NIDA KWA KAZI NZURI YA KUCHAPISHA VITAMBULISHO VYA TAIFA KWA WANANCHI.

 

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imepongezwa kwa juhudi kubwa iliyofanya ya kuchapisha Vitambulisho vingi vya Taifa na kuvisambaza kwa wananchi na hivyo kumaliza kero sugu ya upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Mhe. Vita Kawawa ambaye pia ni Mbunge wa Namtumbo wakati kamati yake ilipofanya ziara kwenye Kituo Kikuu cha Kuchakata na Kutunza Taarifa za Watu cha kukagua mradi wa Vitambulisho vya Taifa NIDA jana. 


"Kamati tumefurahishwa sana na jitihada za Mkurugenzi Mkuu, Menejimenti na watumishi wote wa NIDA katika kuhakikisha mnafikisha malengo ya kuzalisha Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi waliokuwa wamesalia zaidi ya milioni kumi. Hakika mmefanya kazi nzuri na mnastahili pongezi za dhati." alisema


Amesema tatizo la kutopatikana kwa vitambulisho ilikuwa ni kilio cha wananchi kila kona lakini sasa mmezalisha vitambulisho vingi sana na kuvipeleka kwa wananchi katika mitaa, vijiji na vitongoji vyao na hivyo kilio hicho hakipo tena. 

Katika taarifa ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini  kuhusu Utekelezaji wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, iliyowasilishwa kwa niaba yake na  Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Mhandisi Ismail Rumatila,  Naibu Waziri huyo amesema  hadi  kufikia Februari, 2024 NIDA imechapisha jumla ya vitambulisho vya Taifa 20.548,067 na kusambaza vitambulisho 19,743,367 


Amesema kasi ya uzalishaji na usambazaji imeongezeka kutokana na Serikali kutoa fedha za ununuzi wa kadighafi 13,514,251 ambazo zinatumika kuzalisha vitambulisho vya watu wote waliokwishasajiliwa na kupata Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN).


Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa NIDA zilizowezesha kununuliwa kwa kadighafi hizo na hivyo kuchapisha vitambulisho kwa wingi na kuvisambaza kwa wananchi.


Kuhusu kuboresha na kuongeza njia za uhakiki na utambuzi, Mhe. Sagini amesema NIDA inaandaa Mkakati kwa kuongeza uhakiki wa kutumia alama ya mboni za macho na sura ili kuwezesha utambuzi na uhakiki kwa watu wasiokuwa na alama za vidole. Aidha amesema NIDA itaboresha usimamizi wa taarifa na kuboresha uwezo wa kuthibitisha utambulisho wa mtu kipekee.


Amedokeza kuwa, katika mwaka huu wa fedha NIDA imeweka lengo la kukusanya maduhuli ya shilingi 24,000,000.00 ambapo hadi kufikia Februari 2024, imekusanya maduhuli ya shilingi 19,109,275.84 sawa na asilimia 79.6 ya lengo la mwaka huu wa fedha.


“Makusanyo hayo yametokana na tozo za huduma ya ushirikishanaji wa taarifa na huduma za usajili na utambuzi kwa wananchi na wageni wakaazi. Fedha hizi zimewasilishwa Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina” amesema Naibu Waziri Sagini.


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Jumanne Sagini (mwenye tai kushoto) akiwatambulisha Menejimenti na viongozi wengine wa Wizara kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vita Kawawa na wajumbe wengine wa Kamati mara baada ya kuwasili katika Kituo cha uchakataji Taarifa kukagua Mradi wa Vitambulisho vya Taifa jana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi, na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakati Kamati hiyo ilipotembelea Kituo cha Kuchakata Taarifa kukagua mradi wa Vitambulisho vya Taifa jana. Kushoto ni Naibu Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) 


Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi, na Usalama Mhe. Cosato Chumi akizungumza wakati alipokuwa akichangia taarifa ya Utekelezaji wa mradi wa Vitambulisho vya Taifa wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa jana. Kulia anayesikiliza kwa makini ni Mhe.Nicolaus Ngassa Mbunge wa Igunga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments