MAKAMU WA RAIS DK.MPANGO AWAITA WAWEKEZAJI KUJA NCHINI KUWEKEZA,ATAJA FURSA ZILIZOPO

MAKAMU  wa Rais wa Dkt. Philip Mpango amewaita wawekezaji wa Kimataifa kuja nchini kuwekeza kutokana na  mazingira bora zaidi yanayovutia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji yanayotokana na  sera, utulivu, rasilimali na jiografia.

Dkt.Mpango ametoa mwito huo Machi 27,2024 wakati akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo ameyataja baadhi ya maeneo yenye fursa za uwekezaji ikiwemo afya, elimu na miundombinu na kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi.

Kongamano hilo ambalo pia limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali nchini, limejumuisha zaidi ya makampuni mia mbili, sitini yakiwa ni kutoka Mkoa wa Zhejiang nchini China, arobaini yakiwa ni makampuni ya China yaliyowekeza nchini, na makampuni zaidi ya mia moja yakiwa ni kutoka Tanzania.

Kuhusu uwekezaji, Dk Mpango amezisifu kampuni na wafanyabiashara kutoka China kwa kuendelea shiriki maendeleo ya uchumi nchini kupitia uwekezaji wao huku akitoa takwimu mbalimbali za kuongezeka kwa mapato na uchumi.

Ambapo ameeleza katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2023, kituo cha Uwekezaji Tanzania( TIC) kilisajili zaidi ya  kampuni 256 kutoka China, yakiwa na uwekezaji wa takribani Dola za Marekani bilioni B4.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema uukiifuatilia historia ya ushirikiano kati ya Tanzania na China pamoja na uhusiano wa kidiplomasia ambao leo unatimiza miaka 60, hivyo wao Wachina na Watanzania ni ndugu.

Amesema kuwa maendeleo makubwa ya utulivu pamoja na uongozi madhubuti wa Serikali, wafanyabiashara wengi wa China wamevutiwa kuja kuwekeza Tanzania, na zaidi mapokezi wanayopata yanawafanya waendelee kushiriki 

Pia amesema Tanzania ni kiungo muhimu katika ushirikiano kati ya Afrika na China, na hivi Karibuni, Rais Xi Jinping aliweka bayana kuwa Uhusiano wa China na Tanzania  ni ushirikiano namba moja kwa viwango ikilinganishwa na mahusiano mengine ya nchi mbili kati ya China na nchi za Afrika.

"Tuna matarajio makubwa ya Maendeleo ya ushirikiano wa Tanzania na China, ambao misingi yake imejengwa kwenye historia, ujenzi wa ushirikiano wa kiuchumi unaoendelea na urafiki wa kuamainia."

Awali Katibu wa  Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa serikali ya Jinhua nchini China Zhu Chonglie amesema wao kama Mkoa wa Zhejiang, na Serikali yao ya Jiji la Jinhua kama ilivyo katika maeneo mengine ya China na Tanzania wanashiriki kuadhimisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60.

"Mfano mzuri ni Kongamano kubwa la elimu liliratibiwa na chuo chetu cha Zhejiang (Zhejiang Normal University Tanzania China Education Forum)."

Akieleza zaidi amesema elimu ni moja ya maeneo yaliyowasaidia  pamoja kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria ambao unapaswa kuuendelezwa, na ndio maana chuo chao  cha Zhejiang kimewekeza zaidi kwenye mabadilishano ya kielimu na vyuo mbalimbali vya elimu barani Afrika.

Amefafanua mfano mzuri ni  Tanzania  katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia ujenzi wa Taasisi ya Confucius na maktaba Kuu.

Kwenye upande wa Utamaduni pia, amesema Jiji lao na Mkoa mzima wa Zhejiang, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupokea vikundi mbalimbali vya maonyesho ya Utamaduni lakini pia vikundi vya Tanzania vimefika Zhejiang kubadilishana uzoefu.

"Hata ujio wetu hapa kwa ajili ya Kongamano hili la Uwekezaji ni matokeo ya ushirikiano wa kihistoria uliopo lakini na ukuaji unaoendelea, tunapaswa kuutunza kupitia mabadilishano kama haya ya kiuchumi, watu na watu pamoja na kubadilishana uzoefu wa masuala la kisiasa."

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde ametumia nafasi hiyo kuelezea fursa mbalimbali zilizopo nchini na hasa akijikita kuzungumza kuhusu sekta ya uwekezaji ambapo amewaomba wawekezaji kutoka China kuwekeza katika kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema takwimu za sensa ya Watu na Makazi inaonesha Dar es Salaam kuwa na watu wengi na wataendelea kuongezeka hivyo wingi wa watu unapaswa kuwa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. 

Amefafanua Moja ya changamoto ni Makazi hivyo wakati umefika wa kujengwa kwa majengo makubwa kwa kubomoa baadhi ya nyumba zilizopo akitolea mfano baadhi ya nyumba za Kiwalani na Karakata.

"Idadi kubwa ya watu maana yake Makazi ya kuishi yanahitajika , hivyo changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kujengwa majengo makubwa marefu na kisha wananchi wakaishi na huenda ikasaidia kuondoa changamoto ya nyumba kumezwa na  mafuriko.

Pia amesema Dar es Salaam kumekuwa na takataka nyingi, hivyo ni vema kuwa na mfumo utakaowezesha kutabadilisha taka hizo kuwa bidhaa huku akifafanua tayari Kuna Wachina wameanzisha viwanda vidogo kwa ajili ya kubadilisha taka hizo kuwa bidhaa 

Chalamila amesema katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya barabara za mwendokasi kazi,amesema huko nako kuna fursa ambapo wawekezaji wanaweza kuingia ubia na Serikali ya Mkoa na kujenga barabara ambazo watumiaji watakuwa wakilipia na hivyo kuingiza fedha kwa pande zote mbili.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments