SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limemteua Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Mirambo ambae ni Mkufunzi wa Juu wa CAF (CAF Elite Instructor) kufanya ukaguzi wa Mitaala ya Mafunzo ya Makocha nchini Rwanda kabla ya nchi hiyo kuruhusiwa kuendesha kozi ya ukocha ya CAF B Diploma.
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) limetuma maombi CAF kupata idhini ya kuendesha kozi hiyo kwa mara ya kwanza ikizingatia Azimio la Mafunzo ya Ukocha la CAF (CAF Coaching Convention) linalohusu vigezo stahiki.
Hivyo, Mkurugenzi huyo ambaye ni mmoja wa wakufunzi wa juu wa CAF atafanya ukaguzi huo ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo ya kuboresha ambapo ripoti yake ndiyo itakayoonesha kama FERWAFA Itasaini Azimio hilo, na hatimaye kuendesha kozi hiyo.
Ukaguzi huo utafanyika kuanzia Machi 20 hadi 23 mwaka huu. Ni nchi nane tu za Afrika ikiwemo Tanzania ambazo zimesaini Azimio la kuendesha kozi hiyo baada ya kutimiza vigezo husika.
0 Comments