Mwinyi kuzikwa kesho Mangapwani

MWILI wa Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi unatarajiwa kupumzishwa kesho Machi 2, 2024 saa 10: 30 jioni katika kijiji cha Mangapwani visiwani Zanzibar.

Rais Mwinyi amefariki dunia jana Februari 29,2024 katika hospitali ya Mzena iliyopo Kijitonyamana jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.

Akitangaza ratiba ya msiba huo leo Machi Mosi, 2024 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwili wa Hayati Rais Mwinyi utaswaliwa katika Msikiti Mkuu wa Bakwata Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema saa tano na nusu mwili utaondoka nyumbani kwake Mikocheni na kuelekea Msikiti Mkuu wa Bakwata kuswaliwa na sala ya Ijumaa itaongozwa na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Dk Abubakar Bin Zuberi Bin Ally na taratibu zote za kidini.

Aidha, Majaliwa amesema kuanzia saa nane mchana mwili wa Hayati Mwinyi utaelekea uwanja wa Uhuru, dua na salamu mbali mbali za rambirambi zitatolewa na viongozi na wananchi watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho

Amesema, milango ya uwanja wa Uhuru itakuwa wazi kuanzia saa tatu asubuhi hii kwa ajili ya wananchi kuingia kuomboleza pamoja na viongozi wa kitaifa ambao watawasili uwanjani hapo kuanzia saa nne asubuhi kuaga mwili wa Hayati Mzee Mwinyi.

“Kuanzia saa 11 jioni mwili wa Hayati Mzee Mwinyi utaondoka uwanja wa Uhuru na kuelekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya Zanzibar, ” amesema Majaliwa na kuongeza

“Wananchi wa Zanzibar wataupokea mwili wa Mzee Mwinyi uwanja wa ndege wa Abeid Karume kuanzia leo saa 11 jioni na kesho Machi 2,2024 milango ya uwanja wa Amani itakuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi, ” amesema

Amesema kesho saa nne mwili utaondoka nyumbani kuelekea uwanja wa Amani kwa maombolezo ya kitaifa na kuanzia saa 6:30 wananchi na viongozi mbali mbali watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.

Pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza salamu za pole kutoka kwa makundi mbali mbali na atapumzishwa kijijjini Manga Pwani saa 10 jioni.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments