Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida MARTHA MLATA ameagiza Wakala wa Umeme Vijijini - REA kupeleka Umeme kwenye chanzo cha Maji cha Kijiji cha SEMFUNGA ili wananchi wa Kijiji hicho waanze kupata huduma ya Maji na waache kutembea umbali mrefu kufuata Maji.
MLATA alitoa agizo hilo baada ya Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida, kupokea taarifa ya kijiji cha Semfunga wilaya ya Singida Vijijini, ambapo moja ya changamoto iliyotajwa ni shida ya Maji ambayo inasababishwa na chanzo chao cha Maji kukosa Umeme.
Alisema Umeme ni lazima ufike kwenye chanzo hicho cha maji, kama serikali ilivyoagiza Umeme upelekwe kwenye Taasisi zote za umma na maeneo mengine ya kutolea huduma za Jamii.
Aidha MLATA alitia msisitizo kuwa Umeme ni lazima upelekwa kwenye Taasisi zote za Umma, ikiwemo Shule, Vituo vya Afya na Taasisi za Dini.
Awali akisoma taarifa ya kijiji cha SemfungaJOEL PETER ambaye ni Katibu wa CCM Tawi la Semfunga alisema kwa sasa kisma hicho cha maji kinatumia umeme wa Jua (SOLA) hali inayoleta changamoto wakati ambao jua linafunikwa na mawingu au kipindi cha masika.
PETER alisema kutokana na kukosekana kwa umeme kwenye chanzo hicho cha maji Wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata Maji.
Alisema kijiji hicho pia kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa Barabara inayounganisha kijiji hicho na maeneo mengine, na kusababisha wananchi kushindwa kuzifikia baadhi ya huduma za kijamii na wakati mwingine kushindwa kusafirisha mazao yao.
Kamati hiyo ya Siasa Mkoa wa Singida ilitembelea na kukagua Miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kupitia Ilani ya CCM Wilaya ya Singida ikiwemo ujenzi wa Madarasa, Zahanati na Miradi ya Maji na Umeme.
0 Comments