MWANZA. Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa juhudi kubwa anazozionesha za kuruhusu kuendelea ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo inayotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatuma Toufiq, wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo Jijini Mwanza, tarehe 18 Machi, 2024.
“Nimpongeze sana Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mradi huu ulikuwa umesimama kwa muda mrefu, lakini alipoutembelea mwezi Juni 2023, aliwatia moyo na kuwataka NSSF waendelee na mradi huu, akijua utakuwa na tija kwa wananchi wa Mwanza na mikoa ya jirani na kuongeza mapato kwa Serikali,” amesema Mhe. Fatuma.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Neema Mwandabila (Mb), amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa uamuzi wake wa kuruhusu miradi iliyosimama iendelee kutekelezwa. Aidha, ameipongeza NSSF kwa ujenzi wa mradi huo kwani Mkoa wa Mwanza unauhitaji wa hoteli ya aina hiyo.
Naye, Mhe. Mwita Getere (Mb), amesema NSSF ina nidhamu ya hali ya juu hasa katika kutekeleza miradi ya uwekezaji ukiwemo wa hoteli ya nyota tano iliyopo Jijini Mwanza.
Mhe. Mariam Kisangi (Mb) amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa kuhakikisha miradi iliyosimama inatekelezwa na kuwa mradi huo wa hoteli utaleta manufaa kwa NSSF, jamii na Taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliridhia mradi huo uendelee baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Mhe. Profesa Ndalichako amesema mradi huo ulianza tarehe 1 Novemba, 2013 na ulipangwa ukamilike ndani ya miaka mitatu, lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizotokea mradi utakamilika tarehe 30 Desemba, 2024.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa maoni na michango yao ambayo wameichukua na wataenda kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema upo mpango wa kuboresha uwanja wa ndege wa Mwanza ili iwe rahisi watalii kupita kwa wingi na kuiwezesha hoteli hiyo kupata wageni wengi.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake mbalimbali, ambapo kwa upande wa ulipaji wa mafao ya wanachama, wanalipa kiasi kikubwa zaidi ya kile ambacho mwanachama amechangia na ndio maana wanafanya uwekezaji wenye tija.
0 Comments