“Wakinababa tembeleeni watoto wenu”

KATAVI: Baadhi ya wanaume,walezi na ndugu mbalimbali wanaopeleka watoto wanaotokea katika mazingira magumu katika vituo vya kulelea watoto yatima wameombwa kutembelea watoto hao ili kujenga ukaribu na watoto wao wawapo katika vituo hivyo.

Wito huo umetolewa na Sister Rose Sungura mkuu wa kituo cha kulelea watoto waishio katika mazingira magumu cha Mtakatifu Yohana Paul II (matumaini mapya ya watoto) kilichopo Nsemulwa mjini Mpanda alipotembelewa na Shirika la nyumba la Taifa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Sister Rose amesema watoto waliopo kituoni hapo ni kutoka makundi mbalimbali likiwemo la watoto waliofiwa na mama na kubaki na baba, hivyo baadhi ya kinababa wanaopeleka watoto wao kituoni hapo wengi wao huwatelekeza.

“Watoto hawa wanahitaji faraja kutoka kwa ndugu zao,wanahitaji pia kuwafahamu ndugu zao na hata wakikua wanahitaji kuungana na familia zao, hivyo wale kinababa, ndugu, jamaa wanaowaleta hapa ningeomba wasiwatelekeze,wawe wanakuja kuwaona watoto” amesema sister Rose

Nae mmoja wa mzazi mwenye mtoto katika kituo hicho Frank Malambo amesema wanaume wengi hawashiriki ipasavyo kutembelea vituo hivyo hasa pale wanapopeleka watoto wao mara baada ya kufiwa na wenza wao.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la nyumba la Taifa (NHC) Domina Rwemanyila ambaye ni Ofisa Habari shirika hilo amesema kupeleka misaada kituoni hapo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani na ni jukumu la jamii nzima kwani katika watoto hao watapatikana akina mama na akina baba.

Shirika hilo limetoa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili huku idadi ya watoto waliopo katika kituo hicho ni 32 ambapo lengo la kituo hicho ni kutoa malezi, makuzi pamoja na elimu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments