BARABARA IKUNGI_MANG'ONYI KUJENGWA KWA LAMI

 


MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu(CCM), ameitaka serikali kueleza ni lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ikungi hadi Kilimatinde ambayo ina uwezekano wa kuingizia serikali sh. bilioni 150 kwa mwaka kutokana na uwekezaji wa mgodi mkubwa wa madini wa Shanta Gold Mine.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo amesema barabara hiyo ni ya kiuchumi inakatisha katika kata ya Mang’onyi ambayo imebeba mgodi mkubwa wa madini wa Shanta Gold Mine na kwa sababu tayari umeshaanza kumimina dhahabu kwa mwaka unatoa AUNCE 30000 ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 60 sawa na sh.bilioni 150.

Amesema, maana yake ni mapato mengi ya serikali, na kwa sababu mgodi unahitaji pia barabara hii , ni lini serikali kwa kushirikiana na mwekezaji huyo itahakikisha barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 itakamilika, ili kumsaidia mwekezaji kuwa na mazingira mazuri?

Aidha, amesema barabara hiyo inakatisha katikati ya ofisi za wilaya, Mkurugenzi na hospitali ya wilaya.

“Tayari tulishajengewa kilomita 2 ambazo hazijafika kwenye ofisi hizo, nini mpango wa muda mfupi wa serikali kuhakikisha kwamba ofisi ya serikali na hospitali ya wilaya inafikiwa na barabara ya lami,?amehoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema wawekezaji wameenda ofisi ya mkoa na Wizarani kuomba barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.

“Ushauri wako kama ulivyosema tumekuwa tukishauriana kama tulivyofanya Barrick ambao wameamua kutusaidia kujenga CSR hivyo taratibu zitafanyika kuona namna ambavyo tunaweza kusaidiana na Shanta Mine kuweza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami,”amesema.

Aidha, amesema kwakuwa usanifu unafanyika kwenye barabara hiyo tayari maombi ya Meneja wa Mkoa yameshapelekwa kwa serikali kuomba kuendelea kuomba kwa awamu ili ijengwe.

Awali akijibu swali la msingi, Naibu Waziri huyo amesema Zabuni ya manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara ya kutoka Ikungi – Mang’onyi – Londoni hadi Kilimatinde (km 117.8) uko katika hatua za mwisho.

Aidha, amesema Mkataba wa kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina utakuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2024. Kazi za Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina zinatarajiwa kuchukua kipindi cha mwaka mmoja na nusu, hivyo zitakamilika mwezi Disemba, 2025.

“Baada ya Usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha wa ajili ya kuanza ujenzi.”amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments