BUNGE LAPITISHA SH. TRILIONI 1.8 MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI 2024/2025

 -95.28% kuelekezwa kwenye maendeleo

-Serikali kuja na Kanuni ya Uwajibikaji kwa wananchi Miradi ya Mafuta na Gesi Asilia
-Dkt. Biteko aagiza Halmashauri kupeleka fedha za Ushuru wa Huduma vijijini
-Masharti ufunguzi wa vituo vya CNG yarekebishwa kuvutia uwekezaji
-Kapinga atilia mkazo utekelezaji Nishati Safi ya Kupikia na CNG
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha shilingi Trilioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo asilimia 95 ya bajeti hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akijibu hoja mbalimbali za Wabunge ameeleza kuwa, ili wananchi wanaozunguka miradi ya Gesi Asilia na Mafuta wafaidike na rasilimali hiyo Serikali itapitisha kanuni itakayoongoza Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ili kampuni ziweze kuwajibika ipasavyo kwa jamii.
Aidha, kuhusu ushuru wa huduma (service levy) unaotolewa na kampuni za Mafuta na Gesi kwa Halmashauri mbalimbali nchini, Dkt. Biteko ameagiza Halmashauri hizo zihakikishe kuwa sehemu ya fedha hizo zinarudi kwenye vijiji ambapo miradi inatekelezwa.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuja na mpango wa utekelezaji wa service levy ili fedha zinazotolewa ziende pia kwenye maeneo ambapo miradi inatekelezwa, Rais ameshaeleza hataki kuona malalamiko sehemu ambapo Gesi inachimbwa, Service Levy na CSR sasa zitaanza kufanyiwa kazi kwa kasi kubwa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesisitiza kuwa, suala la CSR si siri bali ni kitu cha wazi kwa wananchi na Wabunge hivyo ni haki kwa wananchi hao kupata taarifa za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na kusisitiza kampuni za kitanzania kupewa kipaumbele kwenye miradi ili wananchi wanufaike na rasilimali zilizopo nchini.
Kuhusu hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara miezi kadhaa nyuma, amesema ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa umeme wa megawati 410 lakini sasa uwezo wa kuzalisha umeme umekuwa mkubwa kuliko mahitaji huku mitambo minne ya Kinyerezi ikizimwa na kusubiri changamoto itakayojitokeza.
Amesema kwa sasa kukatika kwa umeme kunaweza kutokea si sababu ya upungufu wa umeme bali baadhi ya miundombinu ya umeme kuchoka kutokana na kuwa ya muda mrefu pia uhujumu wa miundombinu akitolea mfano wizi wa transfoma takribani 87 na nyaya za umeme pamoja na mvua zilizozidi kipimo ambapo mpaka sasa nguzo 651 na transfoma 36 zimeondolewa na maji.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na maboresho ya miundombinu ya umeme pamoja na uwekezaji kwenye miundombinu hiyo ikiwemo ujenzi wa vituo vya kupoza umeme.
Kwa wakandarasi wanaosuasua katika kutekeleza miradi ya umeme nchini ikiwemo kampuni za Serikali kama vile ya ETDCO, Dkt. Biteko amesema watachukuliwa hatua kali ikiwemo za kutowapa tena miradi mingine ya umeme.
Akizungumzia usambazaji umeme vijijini, amesema suala linalotiliwa mkazo na Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji kwanza, kisha vitongoji na baadaye kwenye nyumba na kwamba suala la kuwaunganishia umeme wananchi ni endelevu.
Kwa mikoa iliyo nje ya gridi kama vile Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara ameeleza kuwa mikoa hiyo itaunganishwa na gridi kupitia miradi mbalimbali inayoendelea na hii inajumuisha miradi ya kusafirisha umeme kwenda nchi nyingine za Afrika kama vile Kenya na Uganda.
Kuhusu bei ya umeme kwenye maeneo yanayojulikana kama Vijiji-Miji (Sh. 320,000) amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo la kuyatambua maeneo hayo na uchambuzi umeshafanyika huku maeneo 1,570 yakipatikana hivyo suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali ambapo utaratibu wa malipo kwenye maeneo hayo utaelezwa.
Akizungumzis uanzishaji wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG), Dkt. Biteko amesema suala hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa na sasa masharti ya kuanzisha vituo hivyo yamepunguzwa ambapo wawekezaji wakikamilisha nyaraka zinazohitajika ndani ya Siku Tatu watakuwa wamepata leseni.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati kupitia miradi mbalimbali kielelezo na maendeleo inayoendelea nchini.
Akizungumzia Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Kapinga amesema kuwa, ni nyenzo muhimu ya kusaidia kutunza mazingira na kwamba mkakati wa kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia umeshapitishwa na Baraza la Mawaziri na upo tayari kufanyiwa kazi.
Amesema azma ya Serikali ni kuongeza kasi ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwemo gesi ambapo mkakati una lengo la kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi, salama, endelevu, yenye uhakika pamoja na kuondoa matumizi ya kuni na mkaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge.
Kuhusu gharama za mitungi ya Gesi amesema suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao umeanza kutoa ruzuku ya mitungi na mpaka sasa wameshatoa mitungi 83,500 na mingine 450,000 itatolewa kwa wananchi.
Aidha, kuhusu suala la kuwa na mitungi ya kilo chache ili wananchi waipate kwa gharama ndogo amesema tayari mitungi ya kilo tatu imeanza kuingia sokoni na Serikali inaendelea kusimamia ili kuwa na Mawakala wengi zaidi wa kusambaza gesi hata katika maeneo yaliyo mbali.
Vilevile kuhusu ujenzi wa vituo CNG na vya kubadilsha mifumo ya magari ili kutumia gesi amesema kuwa tayari ujenzi wa kituo mama umeanza katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam, vituo viwili vingine vinajengwa katika eneo la Kairuki na Muhimbili na vingine 20 vitajengwa kwa kushirikiana na Sekta binafsi.
Bajeti ya Wizara ya Nishati iliyoidhinishwa na Bunge ni shilingi 1,883,759,455,000 ambapo Shilingi 1,794,866,832,000 sawa na asilimia 95.28 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Shilingi 88,892,623,000 sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments