MKUU wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Dunstan Kyobya amewataka wananchi ambao nyumba zao zimezingirwa maji ya mvua za mafuriko hususani katika kata saba za Mji wa Ifakara kuondoka na kuhamia maeneo salama ili kunusuru maisha yao.
Kyobya amesema hayo Aprili 25, 2024 wakati akipofanya ziara ya kukagua maeneo ambayo yameathiriwa na mvua za mafuriko ndani ya Halmashauri ya Mji Ifakara .
Amezitaja baadhi ya kata ambazo zimejaa maji ya mvua kwa sasa na nyumba nyingi kuzingirwa na maji ni Viwanja sitini, Mbasa , Mlabani , Katindiuka, Lipangalala , Michenga na Lumemo .
“Wale ambao wanaishi kwenye kata hizi watoke , kuna nyumba ambazo zimejaa maji na tumewaokoa watu ,lakini wengine wanasema mheshimiwa lakini maji tumeyazoea …tunasema tunakuja kuwatoa.. maji hayapimwi kwa kuyaona kwa macho “amesema Kyobya.
Kyobya amesema ,Ofisi ya Maafa ya Waziri Mkuu imeweka kambi wilayani humo kuhakikisha huduma za kibinadamu zinatolewa kwa haraka kwa waathirika wa mafuriko na kuwahakikishia walioathiriwa kuwa chakula kipo cha kutosha na kitalewa kwa kufuata utaratibu uliowekwa .
Amesema kutokana na athari za mvua za mafuriko, amelazimika kulifunga kwa muda daraja la Machipi baada ya maji kujaa na kupita juu yake ili kulinda usalama wa watu na mali zao.
Mkuu wa wilaya ameziagiza kamati za maafa ngazi ya mitaa , vijiji , kata na halmashauri kufanya tathimini zitokanazo na mafuriko hayo katika maeneo yao na na kuwasilisha ngazi ya wilaya ili kupata takwimu sahihi zitokanazo na athari ya mafuriko ya mara kwa mara ndani ya wilaya hiyo.
0 Comments