MARA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amemtaka Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Mchemba na Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata kutupia macho mpaka wa Sirari.
Pia, amewataka kushughulikia adha za wananchi wa mipakani na kuwataka kutumia busara katika kushughulikia matatizo ya wananchi hao.
Mpaka huo unaounganisha Tanzania na Kenya unalalamikiwa na baadhi ya wananchi kupata changamoto ya kuvusha bidhaa na wakati mwingine hata wakiruhusiwa wamekuwa wakitozwa gharama kubwa ikilinganishwa na thamani ya hali ya mzigo waliobeba hali inayowaongezea ugumu wa maisha.
Kinana ameeleza hayo leo Aprili 15 ,2024 katika mkutano wa ndani uliofanyika Tarime Mjini na kusisitiza kuwa hakuna haja ya kuwatesa wananchi kama wanapata bidhaa kwa gharama nafuu.
“Hili ni jambo inabidi nikakae na Waziri wa Fedha na Kamshina wa Mamlaka ya Mapato ili tuelewane na maagizo yatolewe.Kwa sababu mnaweza kuwa na sera nzuri na msimamo alafu watu walioko pale wakawa hawafuati sheria,” amesema.
Kauli ya Kinana imekuja baada ya kusikiliza changamoto za wananchi, zilizotolewa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ambaye amesema kinachofanyika katika mpaka huo bidhaa zinazopatikana Kenya gharama yake ni nafuu ikilinganishwa na Tanzania.
“Simenti ukiitaka ya Kenya na inakuja hadi nyumba kwako unaipata kwa Sh 15,000 hadi Sh 17,000 lakini hapa Tanzania Sh 25,000 kwahiyo kama mwananchi wa kawaida lazima atatafuta nafuu.
“Kama mkulima akienda Kenya mbolea anaipata kwa Sh 50,000 hadi Sh 60,000 hapa Tanzania inaenda hadi Sh 100,000 kuangalia mtu wakijijini tofauti ya Sh20,000 ni hela nyingi,” amesema Waitara
Amesema wananchi wanachokifanya mpakani wameweka utaratibu wanazofanya biashara za jumla wanaruhusiwa kuingiza bidhaa hizo kwasababu wamepewa vibali na wanalipa kodi.
0 Comments