MEWATA WAFANYA MKUTANO WAKE WA 21, WAJIPANGA KUINGIA MKATABA UTAOKASAIDIA AFYA YA MAMA NA WATOTO.

 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amewataka wanachama wa Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala ya ukatlli wa kijinsia hususan ukeketaji kwa watoto.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa 21 wa MEWATA, unaofanyika kila mwaka, Dkt. Gwajima, alisema jambo la muhimu hivi sasa ni kuwafikia wananchi hususan vijijini ambapo idadi kubwa inaonyesha kuwa wengi wao hawapati elimu ya ukatili wa kijinsia.

Alisema zipo baadhi ya sehemu hapa nchini bado wanaendelea kuwakeketa watoto wakike bila kujali madhara wanayoweza kuwapata mabinti hao na kumsababisha kupoteza uhai na hata kukatisha ndoto zao.

"MEWATA jukumu lenu kubwa ni kuangalia namna gani ya kuweza kuifikia jamii kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini niwaombe kuendelea kutoa ushirikiano serikalini kuweza kusaidia suala afya ya mama na watoto inakuwa salama wakati wote. Tukatokomeza

"Tuendelee kuwa na mifumo ya kifikra itakayosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii, wapo ambao wanauana na ndoa kuvunjia lakini mila kandamizi, ukeketaji kwa watoto bado upo hapa nchini, MEWATA ni jukumu lenu kuangalia namna nzuri ya kuifikia jamii na kuitoa elimu,"alisema.

Akitaja tkwimu za ujumla kupitia Ofisi ya Takwimu ya Utafiti wa Demografia na Afya 2015-2016, zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 ya wanawake wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.

Alisema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya Mila na desturi kandamizi ambazo zinazowazuia wanawake na watoto kufikia ndoto zao na kutoa mchango wao katika ustawi wa jamii na Taifa Kwa ujumla.

Mbali na hayo, Dk. Gwajima aliwasihi wanachama wa chama hicho, kuacha kuwa aibu mara wanapopata migogoro yoyote itakayowasilishwa na kuwa wawazi kuwaambia tatizo ni nini ili kusaidia kulitatua mapema.

"Tusione aibu wala kuficha tatizo unapoliona, tunapaswa kusema ukweli utakaosaidia kutatua migogoro itakayojitokeza, nimatumaini yangu katika majukumu yetu ya kazi tutatanguliza kusema ukweli bila kujali tatizo lolote, tuingie mkataba wa kuangalia namna nzuri ya kuisaidia jamii,"alisema.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha MEWATA, Zaitun Bhokhary, alimpongeza Waziri Dk. Gwajima, kwa ushirikiano alioutoa na kuahidi kuwa watatembelea ofisi ya Waziri huyo na kuhakikisha wanaingia mkataba utaokasaidia afya ya mama na watoto.


Akitaja kauli mbiu ya mkutano huo kuwa 'tushirikiane kutoa kipaumbele kwa afya ya wanawake na watoto kwa ustawi wa jamii' ikiwa na lengo kubwa la kukuza mshikamano na uhusiano katika kuhimiza na kukuza utafiti wa kuboresha huduma ya afya kwa wanawake na watoto.

Naye, Makamu wa Rais MEWATA, Dk. Marry Mwanyika, alisema wapo tayari kutoa elimu kwa jamii na kuangalia namna nzuri ya kuweza kuondoa masuala ya ukatili wa kijinsia unaoendelea katika baadhi ya sehemu nchini.

Mratibu wa Kamati ya Haki za afya ya uzazi, kutoka Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Emmanuela Maira, alisema hivi karibuni wataandaa jarida litakalobeba maudhui mbalimbali ya kuielmisha jamii na masuala ya ukatili wa kijinsia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments