WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) unawaomba radhi watumiaji wa kivuko MV. MALAGARASI na wananchi wa Ilagala na Kajeje Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, kutokana na kusimama kutoa huduma kwa kivuko hicho siku ya Tarehe 01 Aprili 2024 majira ya saa sita mchana baada ya kupata hitilafu katika mifumo yake ya uendeshaji na kusababisha injini moja kushindwa kufanya kazi hivyo kivuko kubakia na injini moja. Kivuko hicho kilishindwa kuendelea na safari na kusimama, mabaharia kwa kushirikiana na nahodha wa kivuko walifanikiwa kutia nanga na kukifunga kamba.
Wakati kivuko kinapata hitilafu, kwa mujibu wa taarifa iliyokuwemo katika mashine ya ukatishaji tiketi ambayo inahifadhi kumbukumbu, kilikuwa na jumla ya abiria tisini na tano, gari mbili, moja aina ya Toyota Landcruiser na jingine dogo la abiria TAXI, pikipiki kumi na sita pamoja na baiskeli saba.
Mafundi wa kivuko walifanikiwa kufanya marekebisho madogo ya awali na kivuko hicho kiliweza kutoka eneo la tukio na kufanikiwa kufika katika maegesho majira ya saa kumi jioni na baadhi ya abiria waliokuwepo ndani ya kivuko. Mpaka kivuko hicho kinatia nanga kwenye maegesho, hakukuwa na madhara yoyote kwa abiria wala upotevu wa mali za abiria hao
Juhudi za kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika kivuko MV. MALAGARASI chenye uwezo wa kubeba Tani 50, abiria 100 na magari madogo 6 zinaendelea kufanywa na mafundi wetu hadi wakati huu ili kukirejesha kivuko katika hali yake ya kawaida.
TEMESA inaendelea kuwaomba radhi abiria wote kutokana na changamoto iliyojitokeza na inawakumbusha kuendelea kufuata maelekezo ya mabaharia wakati wote wanapotumia vivuko ili kuendelea kuwa salama.
Imetolewa na Kitengo cha Masoko na Uhusiano TEMESA
02/04/2024
0 Comments