Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida BERTHA NAKOMOLWA amewataka wananchi wa wilaya ya Iramba kuhakikisha wanawalea watoto wao kwa kufuata mila na desturi za kitanzania ili kuepusha changamoto zinazoweza kuwapata ikiwemo Mimba.
NAKOMOLWA alisema hayo wilayani Iramba wakati akizungumza na Wananchi wa wilaya hiyo, akiwa katika Ziara ya Kamati ya Utekelezaji wa Jumuiya hiyo ya Wazazi na Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Wazizi.
Alisema kuwa ni lazima wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa mafunzo na miongozo ya Tamaduni za kitanzania na kiafrika ili waweze kukua kwenye maadili mema.
Aidha alisema kuna baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto zinatokana na malezi mabaya wanayopata kutoka kwa wazazi na walezi.
Katika hatua nyingine NAKOMOLWA aliwataka Wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Alisema ni muhimu kwa kila mwananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili waweze kupata sifa za kupiga kura kipindi cha uchaguzi.
Pia alitoa wito kwa wananchi hasa wanawake kujitokeza kwa wingi kuchukua Fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi huo wa serikali za Mitaa.
Nao Baadhi ya Wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida wakisisitiza kuwa wananchi hao washiri kwa kikamilifu katika uchunguzi huo wa serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.
Hata hivyo wajumbe hao waliwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao.
0 Comments