Wazazi,Walezi Wasisitizwa Kuacha Kutoa Lugha Zisizofaa Kwa Watoto

 

WAZAZI na walezi nchini wamesisitizwa kuacha tabia ya kuwatolea lugha zisizofaa watoto wao wanaofeli masomo na kuwaonesha kuwa hawawezi.

Rai hiyo imetolewa na Mwasisi wa Shule ya Sekondari Huria ya Skillful, Diodorus Tabaro wakati wa Mahafali ya 18 ya Kidato cha Sita, yaliyofanyika shuleni hapo Ukonga ambapo wanafunzi 75 wanatajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu.

Alisema ni vyema mzazi kutumia lugha rafiki kwa Watoto wanaofeli mitihani yao pamoja na kutafuta njia ya kumsaidia ikiwemo kumtafutia shule Huria aweze kuendelea kusoma ili kufikia malengo yake.

“Wazazi waepuke kuwanenea mabaya watoto wao. Kuna wazazi ambao mtoto wao asipofanya vizuri wanaongea nao kwa lugha hasi na kuwaonesha kuwa hawawezi, mdomo wa mzazi ambaye kijana wake anamuona yeye ndo baba au mama, unamuumbia mwanafunzi au kijana husika hivyo kupoteza hali ya kujiamini.

Akizungumzia kuhusu Shule Huria ya Skillful, alisema imefanikiwa kufaulisha wanafunzi 600 kujiunga na vyuo vikuu nchini kwa kipindi cha miaka 18 ya kutoa huduma.

Alisema idadi hiyo ya wanafunzi ni mbali na wale waliojiunga na Vyuo kwa ngazi ya Diploma au cheti na walioamua kujiajiri na kuendelea kutafuta maisha.

Tabaro alisema idadi hiyo kubwa imetokana na hali nzuri ya ufaulu wa wanafunzi wanaopita shuleni hapo ambao hakuna anayepata daraja la nne, isipokuwa kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu.

“Siri kubwa ya sisi kufanya vizuri na kupata wasomi wengi wa vyuo vikuu ni kutoa elimu bora inayomfanya mwanafunzi na mzazi wasijute kuchakua Skillful kwasababu hatutaki arudie kufeli tena mitihani,” alisema Tabaro.

Alitaja mbinu chache za shule hiyo kufanya vizuri kuwa ni walimu kuandaliwa kuwa wazazi, walimu na viongozi wa wanafunzi ili kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo yao.

Mkuu wa Shule hiyo, Allen Maximillian amesema wanafunzi hao wanahitimu kwa kusoma kidato cha sita ndani ya mwaka mmoja katika michepuo yote ya Biashara, Sanaa na Sayansi.

“Tumekuwa na muendelezo wa matokeo mazuri ambao unachagizwa na jitihada za walimu, mazingira pamoja na nidhamu kwa walimu na wanafunzi,” amesema.

Aliongeza kuwa, mafanikio ya shule hiyo pia yanaenda sambamba na ushirikiano na serikali ambao wamekuwa wakiwasimamia bega kwa bega kuhakikisha elimu wanayotoa inakidhi vigezo.

Naye mmoja wa wahitimu hao, Derich Mushenyera, alisema wamejiandaa vyema kufanya mitihani ya mwisho ya kidato cha sita inayoanza wiki ijayo na anaamini watafaulu.

“Maandalizi yalikuwa mazuri, walimu wametufundisha mbinu za kufaulu lakini pia tumefanya mitihani ya mazoezi ya kutosha hivyo tunaamini tupo tayari kwa mitihani na kufaulu vizuri,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments