Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza imeridhishwa na ukamilishwaji wa mradi wa maji wa Butimba na ufanisi wake.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge (Smart) amedhihirisha hayo Mei 27, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua miradi ya maendeleo Wilayani Nyamagana
"Tumefarijika kwa mradi huu wa maji. Mradi ni mzuri, umekamilika na unatoa huduma. Kwa niaba ya Kamati tumeridhika," amesema Lushinge.
Lushinge ameielekeza MWAUWASA kuhakikisha inaharakisha mpango wake wa usambazaji maji ili mradi ulete matokeo yanayokusudiwa sambamba na kuhakikisha usimamizi wa karibu unakuwepo ili mradi uwe endelevu.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Kamati, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Neli Msuya amesema pamoja na kukamilika kwa mradi wa Butimba na kuanza kutoa maji, hatua inayofuatia ni ya kuboresha mfumo wa usambazaji maji kwa kuongeza mtandao wa bomba na kujenga matenki makubwa ya kuhifadhia maji.
"Ili kuhakikisha maji kutoka katika mtambo wa Butimba yanapatikana kwa uwiano sahihi, Serikali kupitia MWAUWASA itatekeleza mradi wa ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji na matenki makubwa matano," amefafanua Neli.
Neli ameainisha maeneo yatakayojengwa matenki kuwa ni Buhongwa (lita milioni 10), Fumagila (milioni 10), Nyamazobe (milioni 5), Kisesa (milioni 5) na Usagara (milioni 1). "Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa Sekta ya Maji kipaumbele cha kipekee," amesema Neli. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Neli, mradi wa Maji Butimba ulianza kutekelezwa Februari 1, 2021 na ulikamilika Oktoba 31, 2023 na unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa MWAUWASA Oktoba mwaka huu.
0 Comments