Na Thobias Mwanakatwe,MANYONI
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk.Emmanue Nchimbi, ameziagiza serikali za mitaa nchini kuwatambua vijana wasomi wa fani mbalimbali ili mikopo iliyopitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuanza kutolewa kwenye halmashauri iweze kuwanufaisha makundi hayo.
Ametoa agizo hilo leo (Mei 29, 2024) katika siku ya kwanza ya ziara yake katika Mkoa wa Singida wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Wilaya ya Manyoni baada ya kumaliza kusikiliza kero za wananchi wa mji huo.
Dk.Nchimbi amesema serikali za mitaa katika utoaji wa mikopo hiyo wazingatie makundi ya vijana wasomi wa fani mbalimbali na kuwapa ushauri wa namna ya kujiunga pamoja na kufanya pamoja.
"Wakati mwingine tuna changamoto hata katika majengo yetu tunayojenga licha ya kuwa na fedha za kutosha lakini viwango vyake vinakuwa vya chini sababu hatuwatumii wataalam wetu,hatuwapi nafasi ya kutumia ujuzi wao," amesema Dk.Nchimbi na kuongeza...
"kuna vitu ambavyo hatufikirii kwanini hatubadiliki mfano wataalam wetu wa kilimo wangetumika vizuri tungeweza kuzalisha alizeti nyingi kuliko sehemu yeyote na pengine Mkoa wa Singida ungeweza kuondoa tatizo la kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi," amesema.
Amesema serikali za mitaa zikitumia mikopo vizuri na utambuzi wa raslimali zetu na nguvu kazi zilizopo nchi yetu itabadilika kwa kasi kimaendeleo.
UKABILA
Akizungumza suala la ukabila, Dk.Nchimbi amewataka Watanzania kuwakataa watu wanaopandikiza mbegu za kuligawa taifa na kila mtu anayezungumzia suala la ukabila atambue kuwa watanzania hawafurahishwi na tabia hiyo.
Amesema wasisi wa taifa hili hawakutaka kuishi Tanzania tu bali walitaka nchi za Afrika Mashariki iwe nchi moja na pia walitaka Afrika iwe nchi moja lakini tumekwama hivyo haiwezekani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umezaa Tanzania turudishwe nyuma na watu wachache wanaoeneza mbegu ya ukabila.
"Katika nchi yetu siku za karibuni baadhi ya watu wameanza kuongelea makabila,wanaongelea bara na Zanzibar,wanaongelea watanganyika, wanasema hatunufaiki na Muungano,wazanzibar hatunufaiki na muungano,kumbukeni safari moja huanzisha nyingine,kila kitu kikubwa duniani kilianza na kitu kidogo,kila vita kubwa duniani ilianza na jambo dogo," amesema.
Dk.Nchimbi amesema mafanikio yaliyopo nchini yanatokana na umoja na mshikamano uliopo hivyo ni muhimu kudumia amani iliyopo.
"Mafanikio haya hakuna ambaye hanufaiki na matunda ya Muungano tulio nao,mafanikio haya tunayapata kutokana na Muungano wa nchi zetu,tusikubali kugawanywa tusikubali kufarakanishwa," amesema Dk.Nchimbi.
Naye Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo,Amos Makala,amesema lengo la ziara hii ambayo ni kuangalia uhai wa chama,maandalizi ya uchaguzi,utekelezaji wa ilani na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
"Tumejiridhisha utekelezaji wa ilani CCM katika Mkoa wa Singida upo imara,tumejiridhisha maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa upo vizuri,wananchi tuendelee kuiamini CCM kwani yapo mambo mengi mazuri ya maendeleo yamefanywa na serikali ya CCM," amesema.
Makalla amesema serikali ya awamu ya sita ndio pekee ambayo imepeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo na kwamba CCM ndio ina wajibu kwa wananchi kuhakikisha inawaletea maendeleo ambapo inafanya hivyo kwa kiwango kikubwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,Martha Mlata, amesema utekelezaji wa ilani katika mkoa huu inakwenda vizuri kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya chama na Serikali.
Mlata alimuomba Katibu Mkuu wa CCM kuingilia kati kusaidia kijengwe kituo cha umeme Manyoni (Substation) ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika wilaya ya Manyoni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida,amesema mkoa huo umepokea Sh.Trilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema ipo miradi mingi inayoendelea kutekelezwa katika huo ukiwamo wa umwagiliaji unaotekelezwa katika wilaya Mkalama kwa thamani ya Sh.bilioni 34.
Dendego amesema katika kuendelea kuimarisha uchumi wa mkoa,serikali imeanza mkakati wa kutangaza vivutio vilivyopo mkoani hapa ambapo hivi karibuni kulikuwa na kikao cha kuzungumzia uwekezaji ambacho kiliendeshwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzanzia (TIC).
Naye Mjumbe wa MNEC Mkoa Singida,Yohana Msita,amesema tatizo la kukatikakatika umeme katika wilaya ya Manyoni limekuwa tatizo sugu na kusababisha malalamiko ya wananchi.
Aidha,Msita ameiomba serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa CCM, kuangalia uwezekano wa kusogeza poli la hifadhi la Kizigo,Muhesi Rungwa kwani ukanda huo una madini mengi hivyo kusogeza kutawapa fursa wananchi kuchimba madini na hivyo kujiingizia kipato.
0 Comments