MADEREVA WATAKIWA KUFATA MIONGOZO YA LATRA KUPANDISHA NAULI.

 

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini - LATRA Mkoa wa Singida, imewataka Madereva na Wamiliki wa vyombo vya Usafirishaji kuacha Tabia ya kupandisha nauli kiholela na baadala yake wafuate sheria za LATRA za upangaji nauli halali.

Kaimu Afisa Mfawidhi  LATRA Mkoa wa Singida IDDY MASHANGA alisema hayo wakati akizungumza na Madereva, Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida wakati wakijadili malalamiko ya Wamiliki hao kuwa nauli zilizopo ni ndogo.
                                      

MASHANGA alisema kuna baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na madereva wamekuwa wakipandisha nauli kiholela kinyume na sheria zilizopo za LATRA za upangaji nauli.

Alisema kuwa endapo Madereva na Wamiliki hao watabainika kupandisha nauli kinyume na utaratibu unaotolewa na LATRA watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupigwa faini.

Aidha MASHANGA aliwataka wamiliki na madereva hao kufuata taratibu zote kama wanaona nauli zilizopo ni ndogo ili LATRA iweze kuangalia malalamiko hayo ili iweze kutoa muongozo mwingine wa ongezeko la nauli.
                                       
Hata hivyo alisema kuwa ili nauli ziongezeke LATRA huzingatia mlipuko wa Bei ya Mafuta na Gharama ya Maisha, hivyo vitu hivyo vikiwa vimepanda basi nauli nazo hupanda au huongezewa kulingana Kilometa.


Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Mkoa wa Singida ELPHAS LWANJI alitoa ushauri kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na Madereva kuhakikisha wanafuata Sheria na taratibu zilizopo ili kupunguza malalamiko ya kupandishwa nauli kiholela.

LWANJI alisema kuna wakati mwingine Madereva hao ndio wanasababisha changamoto hiyo kwa kutoa mwanya kwa Wapiga Debe kukusanya nauli, ambao wanawatoza nauli kubwa abiria.
                                     
Aidha aliwataka pia waanzishe Chama ambacho kitawasaidia kuwa na umoja wa kusimamia masuala yote yanayowahusu katika shuguli zao za usafirishaji.

Wakizungumza katika kikao hicho Madereva na Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji walisema sababu kubwa ya kupandisha nauli kiholela bila kufuta sheria na taratibu za LATRA ni kupanda kwa Bei ya Mafuta.

Madereva na Wamiliki hao wa vyombo vya usafirishaji walilalamikia upangaji wa nauli unaofanywa na LATRA bila kuangalia Gharama na Mazingira ya usafirishaji kwa kupanga nauli kidogo.

Kupanda kwa bei ya mafuta nchini, kumesababisha baadhi ya maeneo madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kupandisha nauli kiholela na kusababisha kero kwa wananchi wanaotumia vyombo hivyo vya usafiri.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments