KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amewasihi Wananchi kisiwani Zanzibar kufuata maelekezo ya kuchukua tahadhari juu ya kimbunga cha ‘’Hidaya’’ yaliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Hayo ameyasema katika mahojiano maalum ambapo ameeleza kuwa kila mwananchi hasa wanaofanya kazi za uvuvi,wanaotumia boti kusafiri bila kujali tofauti za kisiasa wanatakiwa kuzingatia maelekezo ya kusitisha kwa muda kazi hizo ili kuepuka madhara yanayoweza kusabanishwa na kimbunga hicho.
Mbeto, amesema Zanzibar ni nchi ya visiwa hivyo kimbunga hicho kinaweza kuleta madhara makubwa endapo wananchi watapuuza maelekezo ya wataalamu wa masuala ya hali ya hewa nchini.
Katika maelezo yake Mbeto, amefafanua kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaungana na taasisi ya TMA pamoja taasisi nyingine nchini kutoa elimu,nasaha na msisitizo kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya umakini na kufuatilia taarifa za kimbunga hicho kupitia Vyombo vya habari mbalimbali nchini.
“ Chama Cha Mapinduzi tunawaomba wananchi tuzingatie na kuipa kipaumbele taarifa iliyotolewa na TMA ili kuepuka matatizo yanayoweza kusababishwa na kimbunga hiki cha Hidaya kwani sote tunaona hali ya hewa ilivyobadilika katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar”, alisema Mbeto na kuongeza kuwa wazazi na walezi wasiruhusu watoto wao kucheza katika maeneo ya miti,minazi,majengo yenye nyufa au magofu.
Pamoja na hayo, Mbeto alieleza kuwa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imesema hadi kufikia saa 3 ya usiku wa jana Mei 3,2024, kimbunga cha ‘’Hidaya’’ kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilometa 230 kutoka pwani ya kilwa na kilomita 170 kutoka pwani ya Mafia ikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 na kasi ya upepo unaofikia kilomita 120 kwa saa.
Alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo pia imefafanua kuwa Mei 4,mwaka 2024 kinatarajia kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususani mikoa ya Lindi,Mtwara,Pwani,Dar es saalam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo mengine jirani.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Zanzibar Khamis Mbeto Khamis.
0 Comments