Biteko: Walimu tengenezeni taifa la kesho

DODOMA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka walimu  kulitengeneza Taifa kwa kuhakikisha wanazalisha kizazi bora ambacho kitakuwa  na manufaa makubwa kwa Taifa.

Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Juni Mosi, 2024 Jijini Dodoma  wakati akizungumza  na Walimu wa shule za Msingi na Sekondari  za Wilaya ya Dodoma Mjini katika Mkutano uliaondaliwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ambao ulikuwa na lengo la kujadili  changamoto mbalimbali za muhula uliopita na jinsi ya kuzitatua muhula ujao.

“Walimu wana kazi kubwa ya kututengenezea Taifa kwa kutafsiri R4 za  Rais Samia Suluhu Hassan hasa kwenye suala la  maridhiano,”amesema .

Pia, amewataka walimu kujitahidi kuwafundisha kwa umakini ili wanafunzi wazidi kufanya vizuri na kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde katika kuhakikisha elimu bora inatolewa.

Kwa upande wake Waziri wa Madini ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, Anthony Mavunde amesema lengo la Mkutano huo ni kujadili changamoto katika sekta ya elimu katika muhula uliopita na wafanye  nini katika muhula ujao ili kuendelea kuwatia moyo walimu.

“Tuliona njia pekee ya kufanya vizuri ni kuwaweka walimu pamoja hatutaki mwalimu wetu akiwa na changamoto akalalamike kwani haya  ni sehemu ya maisha yetu,”amesema Mavunde

Amesema kupitia mkutano huo watazungumza kwa pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kutatua kero ambazo zitajitokeza.

“Dhamira yangu ni ya dhati katika kukuza elimu kwani nimeweza kujenga shule za msingi na sekondari kwa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu,”amesema Waziri Mavunde.

Amesema kwa kushirikiana na baadhi ya wadau wameweza kujenga uzio katika shule mbalimbali ambao unasaidia watoto kusoma kwa utulivu.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema  Mbunge wa Dodoma,Anthony Mavunde anathamini elimu na kila anapokutana nae huwa anahoji kuhusu miradi mbalimbali ya elimu katika Jimbo la Dodoma Mjini.

Prof. Mkenda amesema kwenye miundombinu Rais Samia Suluhu Hassan wamejenga Vyuo vya Ufundi  (VETA) 64 kwa mkupuo na Campus katika Vyuo Vikuu vyote katika maeneo mbalimbali.

“Tunapoenda kila Mkoa kutakuwa na Campus ya Chuo Kikuu lengo letu ni kuhakikisha elimu inakuwa karibu na wanafunzi,”amesema Prof Mkenda.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments