MTWARA: MWENGE wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara utatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo saba yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 7.7
Akizungumza leo wakati Mwenge huo wa Uhuru ulipowasili katika halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amesema mwenge huo utakimbizwa kwenye umbali wa kilomita 92 katika tarafa mbili, kata sita pamoja na vijiji 12.
Hata hivyo utaweka jiwe la msingi miradi miwili ya maendeleo, kukagua miradi minne na kufungua mradi 1 na miradi itakayotembelewa ikiwemo ya elimu, afya, umeme, shamba la miti la mwananchi na mingine.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”
Mkuu huyo wa wilaya alisema Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 unaendelea kuhamasisha wananchi juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI , Rushwa, Malaria, matumizi ya dawa za kulevya na uzingatiaji wa lishe bora na mengine.
“Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wana hamu kubwa sana ya kuuona mwenge wa uhuru na kuusikia ujumbe wa mwenge”amesema Munkunda
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Eliakim Mnzava ametoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri hiyo kuwa na taarifa sahihi za miradi yote itakayopitiwa na mbio hizo za Mwenge wa Uhuru ili kuthibitisha uhalisia wa gharama za utekelezaji wa miradi hiyo.
0 Comments