Nahodha Taifa Stars amsifu Samia

DAR ES SALAAM – NAHODHA wa timu ya taifa ya soka, ‘Taifa Stars’, Himid Mao amesema ahadi ya Sh milioni 100 ya Rais Samia Suluhu Hassan ilikuwa chachu ya ushindi.

Himid alisema hayo Dar es Salaam baada ya kurejea wakitoka Ndola, Zambia walipokwenda kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 na kuwafunga wenyeji bao 1-0 katika Uwanja wa Levy Mwanawasa.

Kabla ya mchezo Rais Samia aliahidi kutoa Sh milioni 100 endapo Taifa Stars itashinda nje ya Sh milioni 10 ya goli la mama na waliporejea walikabidhiwa hundi ya Sh milioni 100 na fedha taslimu Sh milioni 10.

“Namshukuru Rais Samia na serikali yake kwa kutoa bonasi ya mechi kwa kuwa ilikuwa chachu ya kuongeza ushindi katika timu yetu,” alisema Himid.

Alisema ilikuwa safari yenye mafanikio kwani walipata zaidi ya walichotarajia kwa sababu mchezo ulikuwa ugenini na walishinda na kuwashukuru Watanzania waliokuwa pamoja nao kwa maombi na waliofika uwanjani kuwashangilia.

Naye Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alisema Rais Samia alitoa ahadi mbili na ametimiza zote.

“Mheshimiwa Rais alitoa ahadi mbili, bonasi wachezaji wanalipwa kwenye akaunti zao lakini goli la mama halilali, leo namkabidhi nahodha Sh milioni 10 za goli la mama,” alisema Dk Ndumbaro.

Alisema kuanzia sasa atakayejipendekeza Uwanja wa Benjamin Mkapa atapigwa bao tano ili wachezaji wachukue Sh milioni 50. Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita sawa na vinara Morocco kwenye Kundi E wakitofautiana kwa mabao ya kufunga baada ya kucheza michezo mitatu wote.

Niger inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu sawa na Zambia ambayo imecheza michezo minne lakini Niger wao wamecheza michezo miwili na DRC haina pointi licha ya kucheza michezo miwili.

Kinara wa kila kundi atafuzu moja kwa moja na washindwa bora wanne watacheza mtoano na mshindi atacheza mashindano ya Fifa ya mtoano kuwania nafasi ya kufuzu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments