SERIKALI KUJA NA MKAKATI WA ULINZI KWA WATU WENYE UALBINO

Serikali kuja na Mpango wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino (NAP) kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) na Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa watu wenye ualbino.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kuhusu kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.

Ameongeza kusema Serikali itaendelea Kutoa elimu ya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wakiwemo Watu wenye Ualbino kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Elimu Maalum wa Mikoa yote nchini.

“Tufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Mkakati wake wa Utekelezaji wa Miaka Mitano (National Five Year Implementation Strategy 2024/2025- 2029/2030) na Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miaka Mitano ambayo itazinduliwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha serikali itakamilisha na kuzindua Mkakati wa miaka mitatu 2024-2027 wa Upatikanaji wa Teknolojia saidizi kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino, mkakati huu umepangwa kuzinduliwa mwezi Julai, 2024.

Ambapo ubainishaji na usajili wa watu wenye ulemavu ngazi za kijiji na mtaa kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki na Kazidata ya Watu wenye Ulemavu litaendelea ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu.
Katika hatua Nyingine Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa amesema serikali itaboresha mifumo ya kisheria ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kufuata Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Kanuni za ulinzi wa Mtoto za Mwaka 2015 na Mfumo wa Taifa Jumuishi wa Usimamizi wa Mashauri ya Watoto, Katika kuwahudumia watoto wanaohitaji ulinzi na usalama.

Pia tutanzisha Mfumo wa taarifa Jumuishi wa kitaifa wa kushughulikia Mashauri ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi nchini (NICMS 2017). Hadi Aprili, 2024, jumla ya watoto 708,957 (ME 340,661, KE 368,296) wanaoishi katika mazingira hatarishi wametambuliwa katika Halmashauri zote nchini na kupatiwa huduma kulingana na mahitaji yao.

“Tunatarajia kuanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Halmashauri zote 184 zimepewa jukumu la kutoa elimu, kulinda na kutoa taarifa kuhusiana na ukatili, “alisema Waziri Mkuu.

Ameeleza kuhusu uanzishwaji wa Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto Ndani na Nje ya Shule. Sambamba na Kuanzisha Nyumba Salama kwa ajili ya kuhudumia Wahanga wa ukatili. Ambapo jumla ya Nyumba salama 16 katika mikoa 9 ya Tanzania Bara zimeanzishwa hadi kufikia Aprili 2024;

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments