UTATA MZITO NYUMBA YA MSTAAFU KUBOMOLEWA

                             
MWALIMU mstaafu aliyeitumikia serikali kwa miaka 39 ambaye pia ni mjane, Amina Mghenyi, amemuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa,kuingilia kati kufuatia nyumba yake kutaka kubolewa kwa agizo la mahakama kwa kufuatia kesi iliyotolewa hukumu ambayo hajawahi kuitwa mahakamani hata siku moja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika nyumba hiyo iliyopo eneo la Mahambe kata ya Kibdai Manispaa ya Singida, alisema nyumba yake hiyo imewekewa alama ya X ambayo inatakiwa kubomolewa Juni 16 mwaka huu.

                                 
Alisema kiwanja alichojenga nyumba yake alikinunua Juni 16, 2018 kwa Sh.milioni 17 kwa marehemu John Gwau na kupewa hati namba 573 ambapo tangu alipokinunua na kujenga nyumba amekuwa akikilipia halmashauri kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.

Amina alisema katika hali ya kushangaza Mei 31, 2024 nyumba yake iliwekewa alama ya X na dalali wa mahakama wa kampuni ya Taomtra Limited ambapo anatakiwa kuibomoa mwenyewe Juni 15, 2024 na asipofanya hivyo ifikapo tarehe hiyo litapelekwa geleda na kuibomoa.

Alisema kinachomshangaza ni kwamba kesi ambayo ilipelekwa mahakamani na mlalamikaji Suzana Mahami kuhusu kiwanja cha nyumba hiyo yeye hajawahi kuitwa mahakamani na wala hakuwa mshitakiwa katika kesi hiyo.

Naye Suzana Mahami ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo alisema ni kweli mwalimu huyo hakuhusika katika kesi aliyoipeleka mahakama ya ardhi bali alimshtaki aliyeuza kiwanja hicho palipojengwa nyumba ya mwalimu huyo kwa kuwa aliuziwa eneo hilo kinyume.
                               

Alisema kimsingi mwalimu huyo kesi hiyo imemugusa kwasababu amejenga nyumba yake katika kiwanja ambacho kilikuwa na mgogoro bila yeye kujua.

"Mimi kimsingi sina tatizo na mwalimu huyo nachotaka kama atataka nilipwe gharama zangu za kesi na kupewa kiwanja kingine halafu mimi nitamuachia eneo hilo alipojenga nyumba yake," alisema Suzana.

Naye Sixmund Gwau ambaye ni mtoto wa John Gwau aliyeuza kiwanja hicho kwa mwalimu huyo mstaafu alisema baba yake alipouza eneo hilo hakukuwa na mgogoro  wowote bali mwalimu huyo aliuziwa kihalali kabisa kwa kufuata taratibu zote.

Naye Balozi wa mtaa wa Mahembe, Asia Hamis, alisema serikali iangalia namna ya kumsaidia mwalimu huyo mjane kwani kama nyumba yake itabomolewa familia yake ataipeleka wapi na amezeeka hana nguvu za kuweza kufanya kazi kupata pesa za kujenga nyumba nyingine.

Diwani wa kata ya Kindai, Imari Hamis, alisema tangu 2015 alipoingia kwenye udiwani hajawahi kusikia eneo hilo lina mgogoro na kwamba kinachoshangaza hukumu ya kesi hiyo ilitolewa tangu 2012 halafu utekelezaji wake unakuja kufanyika mwaka huu kitu ambacho kinatia mashaka.

                          
"Naiomba serikali  na mahakama imsaidie mjane huyu kuokoa maisha yake kwani nyumba yake ikibomolewa na hali aliyokuwa nayo ni wazi kuwa kutasababisha maisha yake kuwa magumu sana," alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Singida,Bahati Colex, alisema hukumu ya kesi hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Kuu Dodoma na wao walipewa oda na kumtafuta dalali wa mahakama kwa ajili ya kutekeleza kuibomoa nyumba hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Taomtra Limited, Salimu Adamu alisema wao kama madalali wa mahakama walipewa kazi hiyo ya kutaka kubomoa nyumba hiyo na Baraza la Ardhi.
 Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments